Hivi karibuni, timu ya wanasayansi toka Taasisi ya Francis Crick iliyopo Chuo kikuu cha London, imebaini jinsi uchafuzi wa hewa unavyochochea maradhi ya saratani ya mapafu kwa watu wasiovuta sigara, ambapo kwasasa wanaendelea kutafuta njia za kusaidia kuzuia, kugundua na kutibu ugonjwa huo.

Matokeo hayo, ambayo bado hayajachapishwa katika jarida lililopitiwa na rika, yaliwasilishwa katika mkutano wa kila mwaka wa Jumuiya ya Ulaya ya Oncology ya Matibabu jijini Paris, na kufichua jinsi chembe ndogo zinazozalishwa na moshi wa magari, zinavyokuza seli za mapafu ambazo zina mabadiliko yanayosababisha saratani.

Licha ya kutochapishwa, lakini yamesaidia kueleza kwa nini watu wengi wasiovuta sigara wanaugua saratani ya mapafu, na wanaweza kutoa dalili za kupata uvimbe kama huo, ambapo imebainika uvutaji wa hewa chafu, itokanayo na vyombo vya moto na mashine za aina tofauti.

Ugonjwa wa Saratani ya Mapafu unaotajwa kusababishwa na athari za ufutaji wa hewa chafu kwa wasiovuta sigara. Picha na Vaidan.com

Kiongozi wa mradi, ambaye ni Profesa wa dawa binafsi za saratani katika Chuo Kikuu cha London, Charles Swanton anasema, “Utafiti wetu umebadilisha kimsingi jinsi tunavyoona saratani ya mapafu kwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara.”

Anaongeza kwamba, “Seli zilizo na mabadiliko yanayosababisha saratani hujikusanya kiasili tunapozeeka lakini kwa kawaida hazifanyi kazi na tumeonesha kuwa uchafuzi wa hewa huamsha seli hizi kwenye mapafu, na kuzihimiza kukua na uwezekano wa kuunda tumors.”

Wanasayansi hawa, walichambua data kuhusu mfiduo wa PM2.5 na saratani ya mapafu katika watu 400,000 kutoka Uingereza, Taiwan, na Korea Kusini na kufanya majaribio ya kimaabara kwa kutumia panya, seli za binadamu na tishu na kupata matokeo hayo.

Uvutaji wa Sigara unatajwa kuwa ni moja ya sababu zinazochangia upataji wa Saratani ya mapafu. Picha na vagcel.ru

Wanasema, viini viwili vya kansa za kimazingira, moshi wa tumbaku na mwanga wa urujuanimno huharibu DNA na kuunda mabadiliko ambayo hutoa uvimbe ingawa hawakupata ushahidi kwamba chembe za PM2.5 zinabadilisha moja kwa moja DNA, na bado wanatafuta maelezo tofauti.

Hata hivyo, wanabainisha kuwa waligundua kuwa chembe hizo zilisababisha kuvimba, au kuanzisha mabadiliko ya awali katika jeni ambayo huendesha maendeleo ya saratani nyingi za mapafu, na matokeo hayo yanaweza kutumika kwa saratani nyingine zinazohusiana na uchafuzi wa hewa, ikiwa ni pamoja na mesothelioma, uvimbe wa koo na mdomo.

Uvutaji sigara, bado unatajwa kuwa ni sababu kuu ya saratani ya mapafu, ambapo mwaka 2019, vifo 300,000 ulimwenguni vilihusishwa na mfiduo wa PM2.5 ambazo ni chembe ndogo zinazopatikana kwenye moshi wa gari kitu kilichopelekea kufanyika kwa utafiti huo.

Wanasayansi wanasema moshi utokanao na magari, husababisha Saratani ya mapafu kwa wasiovuta sigara. Picha BBC

Mtafiti Emil lim ayeye anasema, “Asilimia 99 ya watu duniani wanaishi katika maeneo ambayo yanavuka mipaka ya kila mwaka ya Shirika la Afya Ulimwenguni kwa PM2.5, ikisisitiza changamoto za afya ya umma zinazoletwa na uchafuzi wa hewa kote ulimwenguni.”

Uchafuzi wa hewa umehusishwa na matatizo mengine ya afya, ikiwa ni pamoja na pumu, ugonjwa sugu wa mapafu ya kuzuia (COPD), ugonjwa wa moyo, na shida ya akili. Jinsi inavyosababisha saratani kwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara imekuwa siri kwa muda mrefu.

Prof. Swanton, yeye anasisitiza umuhimu wa kuepuka uchafuzi wa hewa. ili kupunguza hatari ya magonjwa na kusema utafiti huo ulifadhiliwa na Taasisi ya Utafiti wa Saratani ya Uingereza kama sehemu ya juhudi pana za kuelewa jinsi saratani ya mapafu inavyoanza na kuibuka kwa matumaini ya kupata matibabu mapya ya ugonjwa huo.

Ramaphosa 'ajipa' usuluhishi vita ya Urusi na Ukraine
Bungeni: Serikali yakanusha Samaki kuhifadhiwa kwa dawa za maiti