Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira jana aligeuka mbogo na kupambana na waandishi wa habari waliokuwa wakijaribu kumpiga picha, muda mfupi baada ya Mahakama kutupilia mbali maombi yake ya kukata rufaa dhidi ya kesi ya kupinga matokeo ya Ubunge wa jimbo la Bunda Mjini.

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa Wasira ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika alijaribu kumvamia mpiga picha wa gazeti la Mwananchi aliyetajwa kwa jina la Jamson akitaka kumnyang’anya kamera ili afute picha alizokuwa anampiga.

“Njoo, njoo hapa wewe kijana. Nakuambia futa hizo picha kwa usalama wako. Nakuambia futa hizo picha. Hivi mnanitafuta nini maana mnanifuatilia tangu nikiwa kule Mahakama Kuu hadi huku,” Wasira anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

Mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Judidhi Nyange alieleza kuwa baada ya kushindwa kumnyang’anya kamera, Wasira alijaribu kumgonga na gari lake wakati anaondoka kwa hasira lakini alishindwa. “Baadae, Wasira alitaka kumgonga na gari wakati anaondoka lakini ilishindikana.”

Wasira aliyekuwa anatetea nafasi yake ya Ubunge wa jimbo la Bunda Mjini kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa tiketi ya CCM, alishindwa na Esther Bulaya aliyewania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema.

Wapiga kura wake walifungua kesi ya kupinga matokeo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza lakini Mahakama hiyo iliitupilia mbali.

Sumaye amvutia Magufuli Upinzani
Habari Mpasuko: Naibu Spika, Dk. Tulia anusurika kifo baaa ya kupata ajali