Saa chache baada ya Msimamizi wa Uchaguzi kumtangaza Ester Bulaya wa Chadema kuwa mshindi katika jimbo la Bunda Mjini, aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo na mpinzani wake mkuu Stephen Wassira amejitokeza na kupinga matokeo hayo.

Wassira amedai kuwa matokeo hayo sio halali na kwamba kuna hujuma zimefanywa ili kumuangusha na kumpendelea Esther Bulaya.

Wassira ambaye pia alikuwa Waziri wa Chakula na Ushirika, amedai kuwa matokeo yaliyotangazwa yana kasoro kubwa ikiwa ni pamoja na idadi ya kura zinazoonekana kuwa zilipigwa zinazidi jumla iliyopo kwenye matokeo hayo.

Alisema kuwa msimamizi wa uchaguzi alimhujumu kwa kuongeza tarakimu kwenye matokeo hayo na kwamba tarakimu hizo zilipelekea idadi ya wapiga kura kwenye kituo kimoja kuzidi idadi iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mwanasiasa huyo mkongwe pia amedai kuwa msimamizi wa uchaguzi alitangaza matokeo bila kuzingatia sheria ya uchaguzi.

Ester Bulaya na Wassira ni mahasimu wakubwa wa kisiasa ambao walianza ushindani mkubwa katika jimbo hilo tangu Ester Bulaya alipokuwa mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM.

Wabunge Waliotangazwa Jioni Hii
CCM Na Chadema Waibuka Tena Majimbo Mkoa Wa Mara