Msanii wa filamu nchini, Wastara Issa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonyesha moyo wa kuguswa na tatizo linalomsumbua na kuweza kumpatia kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya matibabu ya mguu pamoja na mgongo.

Wastara ametoa shukrani hizo Jijini Dar es Salaam alipokua akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa awali ilikua aondoke nchini tarehe 28 mwezi januari mwaka huu kwenda mjini Mumbai kwa ajili ya matibabu lakini kutokana na baadhi ya mipango kutokaa vizuri safari hiyo ilisogezwa hadi jumapili tarehe 4 Februari 2018.

Amesema kuwa katika safari hiyo ataongozana na nesi mmoja kutoka hospitali ya TMJ pamoja na mtu mmoja kutoka katika familia yake ambapo matibabu yake yatafanyika katika hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai na kutarajia matibabu hayo kuchukua takribani wiki tatu na zaidi.

Aidha msanii huyo ameishukuru wizara inayosimamia Tansia ya filamu kwa kumfariji katika kipindi hiki kigumu anachopitia huku akimshukuru Waziri mwenye dhamana na tasnia ya filamu nchini, Bodi ya Filamu Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na watanzania wote kwa kuonyesha upendo wa dhati kwake.

“Asanteni sana Watanzania mmeonyesha moyo wa dhati kwangu kwa muda mrefu sasa, mmekua pamoja nami tangu kipindi cha matibabu ya Sajuki hadi sasa, uzito wa neno asante kutoka kwangu leo hauwezi kulipa fadhila kwa dua na michango yenu kwangu, mwenyezi mungu aendelee kuifanya nchi yetu kuwa na amani na upendo” amesema msanii Wastara Issa

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Joyce Fissoo amesema kuwa serikali kupitia bodi ya filamu inashukuru kwa kupata taarifa kamili ya safari ya msanii Wastari Issa ilipofikia kwani bodi ya filamu inapenda kumuona Wastara akiwa katika afya nzuri na kurudi katika hali yake ili aweze kuungana na wanatasnia wenzake kuendeleza tasnia ya filamu nchini.

Bibi. Fissoo amesema kuwa Watanzania wengi wamekua wakiwasiliana na Wastara kwa njia mbalimbali, kumchangia na hata kufika kumuona, hivyo serikali inatambua kuwa msanii Wastara Issa yupo katika maandalizi ya safari ambapo awali alikua asafiri  tarehe 28 mwezi januari mwaka 2018 lakini kutokana na taratibu za safari kutokukamili kumepelekea safari hiyo kusogezwa hadi tarehe 4 februari mwaka huu.

LIVE: Rais Magufuli katika maadhimisho ya wiki ya sheria
Tanzia: Msanii Radio afariki dunia