Watafiti watatu wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian kilichoko mkoani Arusha wameuawa kikatili jana na wananchi wilayani Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kupigiwa yowe wakidhaniwa kuwa ni wanyonya damu.

Imeelezwa kuwa watafiti hao waliokuwa wakitumia gari ya Serikali yenye namba za usajili STK 9570 aina ya Toyota Hillax, waliuawa kikatili na gari hilo kuchomwa moto baada ya wanawake wa kijiji cha Iringa-Mvumi wilayani humo kuwapigia yowe wakihisi ni wanyonya damu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kuwa Jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa akiwemo mwenyekiti wa kijiji cha Iringa-Mvumi.

Alisema kuwa mwenyekiti huyo wa kijiji ni mmoja kati ya waliohusika kuwashambulia wataalam hao wa kilimo hadi kufa baada ya kufika katika eneo la tukio na kutoyaamini maelezo ya wataalam hao.

Imeelezwa kuwa wataalam hao waliokuwa wakizunguka kijijini hapo walipotea njia, ndipo walipoingia katika eneo ambalo waliwakuta wanawake kadhaa wakichimba chumvi na kujaribu kuwauliza uelekeo lakini waligeuka mbogo na kuwapigia yowe.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simo Kawea alieleza kuwa baada ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano kuwakamata watafiti hao, walioneshwa baadhi ya vielelezo vya vya kuwaruhusu kufanya utafiti katika eneo hilo lakini walikataa na kuendelea kuwashambulia hadi kifo.

“Hata walipooneshwa vielelezo kwamba wao sio wezi bali ni watafiti, wanakijiji hao walikataa na kuendelea kuwashambulia,” alisema Kawea.

Aliongeza kuwa polisi waliwasili katika eneo hilo na kukuta wataalam hao wameshambuliwa vibaya, walijaribu kupiga risasi juu lakini walizidiwa nguvu na wanakijiji hao na kuamua kukaa pembeni wakisubiri msaada wa nguvu zaidi.

Mkurugenzi wa utafiti wa Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi, Anuari Mafuru ambaye mwanae pia (Faraj Mafuru) aliuawa, alieleza kusikitishwa na tukio hilo akisema kuwa waliouawa wote ni wataalam, mmoja akiwa katika mafunzo na dereva ambaye pia alikuwa na utaalam wa utafiti huo.

Gereza la kitengule Kagera, JPM aagiza wasipewe fedha yoyote watetemeke na kufanya kazi
Video Mpya: Barakah Da Prince feat. Ali Kiba - Nisamehe