Wachezaji vijana Victor Osimhen na Samuel Chukwueze wametajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria, itakayoingia kambini baadae mwezi ujao, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika 2019, dhidi ya Afrika kusini.

Hii ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji Osimhen anaecheza kwa mkopo kwenye klabu ya Sporting Charleroi ya Ubelgiji akitokea Wolfsburg Ujerumani na Chukwueze wa Villarreal ya Hispania kuitwa kwenye timu ya taifa ya wakubwa.

Wachezaji hao vijana wenye umri wa miaka 19 kila mmoja, walikua sehemu ya timu ya taifa ya vijana ya Nigeria chini ya umri wa miaka 17 iliyoshiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2015.

Nahodha na kiungo John Mikel Obi, bado anaendelea kuwa nje ya kikosi cha Nigeria, kufuatia sababu binafsi, huku kiungo wa klabu ya Leicester City Wilfred Ndidi akiachwa kutokana na kuonyeshwa kadi mbili za njano katika michezo iiliyopita ya kuwania kufuzu fainali hizo.

Kabla ya kutangaza kikosi kitakachoivaa Afrika kusini, kocha mkuu wa Nigeria Gernot Rohr aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Tumeamua kuwapa nafasi wachezaji vijana Osimhen na Chukwueze, na nahodha wetu Mikel Obi atarejea kikosini, pindi atakapomaliza matatizo yake binafsi,”

Kwa upande mwingine mchezaji mwenye uzoefu Ogenyi Onazi ameachwa kufuatia majeraha yanayomkabili katika kipindi hiki, huku beki Adeleye Aniyikaye akiitwa kwenye kikosi hicho, ambacho kitapambana vikali mjini Johannesburg, Novemba 17.

Siku tatu baada ya mchezo huo, kikosi cha Nigeria kitacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Uganda, kwenye uwanja wa Stephen Keshi uliopo mjini Asaba.

Kikosi cha wachezaji 23 kilichotajwa, kwa ajili ya maandalizi ya mpambano dhidi ya Afrika kusini (Bafana Bafana).

Makipa: Francis Uzoho (Elche, Spain); Ikechukwu Ezenwa (Enyimba) na Daniel Akpeyi (Chippa United, South Africa)

Mabeki: Olaoluwa Aina (Torino, Italy); Adeleye Aniyikaye (FC IfeanyiUbah); Semi Ajayi (Rotherham United, England); Bryan Idowu (Lokomotiv Moscow, Russia); William Ekong (Udinese, Italy); Leon Balogun (Brighton & Hove Albion, England); Kenneth Omeruo (Leganes, Spain) na Jamilu Collins (SC Padeborn, Germany).

Viungo: Oghenekaro Etebo (Stoke City, England); John Ogu (Hapoel Be’er Sheva, Israel) na Mikel Agu (Vitoria Setubal, Portugal)

Washambuliaji: Ahmed Musa (Al Nasr, Saudi Arabia); Kelechi Iheanacho (Leicester City, England); Moses Simon (Levante, Spain); Victor Osimhen (Royal Charleroi SC, Belgium); Odion Ighalo (Changchun Yatai, China); Alex Iwobi (Arsenal, England); Samuel Kalu (Bordeaux, France); Isaac Success (Watford, England) na Samuel Chukwueze (Villarreal, Spain)

Wachezaji waliotajwa kwenye orodha ya pembeni (Standby): Henry Onyekuru (Galatasaray, Turkey); Chidozie Awaziem (Porto, Portugal); Nyima Nwagua (Kano Pillars); Sunday Adetunji (Enyimba) na Junior Lokosa (Kano Pillars)

Nigeria inaongoza msimamo wa kundi E, kwa kuwa na alama tisa baada ya kucheza michezo minne, wakifuatiwa na Afrika kuisni wenye alama nane.

Endapo watafanikiwa kuifunga Afrika kusini katika mchezo wa Novemba 17, mabingwa hao mara tatu wa barani Afrika, watakata tiketi ya kucheza fainali za Afrika, zitakazounguruma nchini Cameroon mwaka 2019.

RADO watangaza hukumu ya Mohamed Issa "Banka"
Marekani yataka kusitishwa kwa mapigano Yemen

Comments

comments