Kamati ya ufundi la klabu ya Njombe Mji jana (Jumatatu) ilikamilisha zoezi la kuwafanyia usahili wachezaji waliojitokeza kwa ajili ya usajili wa msimu wa 2017/18 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara ambao utaanza rasmi mwezi Agusti.

Afisa habari wa Njombe Mji Solanus Muhagama, amesema kukamilika kwa zoezi hilo, kunatoa nafasi nyingine kwa viongozi wa juu wa klabu hiyo kufanya mazungumzo na wachezaji waliopitishwa.

Hata hivyo amesema mbali na wachezaji waliofanyia usahili na kuonekana wanafaa kusajiliwa, pia watafanya usajili wa wachezaji wengine waliopendekezwa na benchi la ufundi.

“Kwa sasa itakua mapema mno kutangaza majina ya wachezaji tuliofanikiwa kuwapata baada ya zoezi la kuwafanyia usahili, hatuwezi kufanya hivyo mpaka tutakapomalizana nao.

“Katika kipindi hiki kila klabu imekua ikisubiri jina la mchezaji fulani litajwe ili waanze kufanya fitna za kumsajili, kwetu hatutofanya kosa hilo kabisa, tunaamini wachezaji tulinao wana uwezo mkubwa kisoka.” Amesema Solanus

Wakati huo huo Solanus Muhagama amesema wanaendelea kuridhishwa na utendaji kazi wa kamati ya mipango na fedha ambayo waliiunda kwa ajili ya kutafuta vyanzo vya mapato yatakayoweza kusaidia katika heka heka za ushiriki wao kwenye ligi kuu msimu ujao.

“Tuna imani kubwa sana na kamati yetu ya fedha na mipango, tangu ilipoteuliwa imekua ikifanya kazi zake kimya kimya kwa sababu muda tuliowapa unatosha kufanya shughuli zao kwa nafasi.

“Kuna baadhi ya mambo wameanza kuyaonyesha na kuuridhisha uongozi wa Njombe Mji FC ambayo yatatuwezesha kuwa na vyanzo kadhaa vya mapato, Moja wapo ni ubunifu wa jezi za klabu ambazo zitakuwa na mvuto wa kununuliwa na shabiki yoyote hapa nchini.”

Njombe Mji itashiriki kwa mara ya kwanza ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2017/18, baada ya kupanda daraja ikitokea ligi daraja la kwanza msimu wa 2016/17.

?LIVE: Rais Magufuli akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara Kibaha
Rais Mstaafu Olusegun Obasanjo wa Nigeria ampongeza Rais Dkt. Magufuli