Watu watano wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya gari lenye namba za usajili T.111 CUU aina ya Mitsubish Fuso kugongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T.612 BNN aina ya Mitsubish Canter  katika eneo la Konoike kijiji cha Kolila wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo Septemba 08, 2021 majira ya saa 10:00 alfajiri huko Barabara ya Arusha/Moshi eneo la Konoike na kusababisha vifo hivyo.

ACP Masejo amesema uchunguzi wa awali umebaini kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha ambapo ilihama upande wa pili wa Barabara na kugongana na gari aina ya Mitsubish Canter lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Moshi. 

Waliofariki katika ajali hiyo ni Peter Mmasi  ambaye ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi Canter, Victor Kileo ,  Vivian Urio  na Isack Temba ambao walikuwa abiria wa gari aina Mitsubishi Canter na ni wakazi wa Baraa jijini Arusha  na katika gari aina ya Mitsubish Fuso aliyefariki ni utingo wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina moja la Idd mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro.

Aidha Majeruhi katika ajali hiyo ni Heriel Jinja Lyimo ambaye amepelekwa katika hospitali ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Jijini Arusha.

Hata hivyo ACP Justine Masejo  ametoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini na matumizi sahihi ya alama za usalama Barabarani ili kuepusha madhara makubwa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai na uharibifu wa  vyombo vya moto wanavyotumia.

Majaliwa atoa maagizo kwa Mawaziri na Makatibu wakuu
IFM kuipa Tanzania trilioni 1.3