Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Waryoba, Hamfrey Polepole ameupinga wimbo wanaoimba wanasiasa wengi hivi sasa, ‘Watanzania Wanahitaji Mabadiliko’.

Wimbo huo unaoimbwa hasa na viongozi wa vyama vya upinzani wakimaanisha kuwa watanzania wanahitaji kubadili utawala uliopo ili wayapate mabadiliko wanayoyataka na kwamba tatizo sio mtu bali tatizo ni mfumo.

Akiongea katika kipindi cha Mada Moto cha Chanel Ten, Hamfrey Polepole ambaye alikuwa akijadili mada ya ‘Kuelekea Uchaguzi Mkuu’ akiwa na Joseph Mtatiro.

Polepole alisema kuwa kutokana na uzoefu alioupata wakati anazunguka kukusanya maoni ya watanzania kuhusu katiba mpya, aligundua kuwa watanzania hawahitaji mabadiliko bali wanahitaji ‘Mageuzi’.

“Watanzania hawahitaji Mabadiliko kwa maana ya ‘Change’, wanahitaji Mageuzi kwa maana ya ‘Transformation’. Unajua mabadiliko ni sehemu ndogo sana ya maguezi, mageuzi ni sehemu kubwa sana inayobeba mabadiliko ya mfumo na mengine mengi. Tukisema watanzania wanahitaji mabadiliko kwa maana ya kubadili chama tawala tunakosea. Watanzania wanahitaji zaidi ya hilo.”

Katika hatua nyingine, Polepole alisisitiza kuwa watanzania wanapaswa kutowachagua wagombea ambao wana tuhuma za ufisadi akimtolea mfano mgombea wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa.

Kwa upande wake Joseph Mtatiro, alisema alipingana na Polepole akidai kuwa mfumo wa Chama Cha Mapinduzi ndio tatizo kubwa linaloitafuta Tanzania na sio mtu mmoja. Hivyo, kumtoa mtu mmoja mmoja kwenye mfumo sio tiba ya tatizo.

Mtatiro alitoa mfano kuwa katika serikali ya awamu ya Pili iliyoongozwa na Ali Hassan Mwinyi, ufisadi na rushwa uliibuka lakini ulizidi hasa baada ya kuondoka yeye na kuingia rais Mkapa ambaye awali alipigiwa debe na Hayati Mwalimu Nyerere kuwa ni msafi.

Aliongeza kuwa hata wakati Rais Kikwete anaingia madarakani serikali yake ilikuwa safi lakini mfumo uliichafua na kusababisha kuibuka kwa ufisadi kuzidi awamu zilizopita. Hivyo, mfumo ndilo tatizo la kwanza na sio mtu mmoja mmoja.

Akizungumzia kuhusu tuhuma, Mtatiro alieleza kuwa wagombea wote wa urais wana tuhuma kwa kuwa Lowassa ana tuhuma ya ‘Richmond’ na Magufuli ana tuhuma ya ‘Nyumba za Umma’.

 

Wizkid Kufanya Remix Ya Wimbo Wa AY
Kiwanda Cha Nyama Ya Punda Chabainika Dodoma, NEMC Wacharuka