Watanzania leo wanaadhimisha miaka 55 ya Uhuru huku viongozi kutoka nchi mbalimbali wakitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo.

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza  chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli ambapo mwaka jana alisitisha  sherehe hizo na kuamua fedha zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya shughuli hiyo ya kujenga barabara ya Bagamoyo kutoka Morocco, Kinondoni hadi Mwenge.

Aidha, kwa taarifa iliyotolewa na  Waziri wa Nchi na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amewataka wananchi wote kushirikiana  na kusherekea  Uhuru wa Tanzania bara kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano ya kupinga ufisadi na rushwa nchini.

“Kwa niaba ya Serikali  natoa wito kwa wananchi wote nchini  kusherekea siku hii kwa kuwakumbuka waasisi waliotetea na kutuletea Uhuru wa nchi yetu, niwaombe wananchi wote kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dk. John Magufuli katika kuimarisha uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”amesema Mhagama.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli

Kwa upande wake  Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limejipanga kuhakikisha  amani na utulivu vinatawala katika maadhimisho hayo yanayofanyika leo  uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.

“Tunaomba wananchi wasiwe na wasiwasi wowote wa kiusalama na pia wajitokeze kwa wingi uwanjani  ili kusherekea sikukuu hiyo kwa utulivu na amani”amesema Sirro.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha  sherehe hizo ni “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa  na Ufisadi na Tuimarishe Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo yetu”

Mbarawa: TCRA tokomezeni wizi mtandaoni
Video: Mambo ya muhimu yakufahamu kuhusu BIMA