Serikali imesema tayari imepeleka muswada wa mabadiliko ya sheria itakayo ruhusu wananchi kujipima wenyewe maambukizi ya Virisi vya Ukimwi kwa kutumia mate wawapo majumbani.

Akizungumza jana katika ufunguzi wa semina yenye lengo la kuwajengea uelewa wasanii juu masuala ya Virusi vya Ukimwi (VVU), na Ukimwi, Waziri wa wizara ya Afya, Ummy Mwalimu, amesema changamoto kubwa katika kukabiliana na kutokomeza maambukizi ya Ukimwi ni watu kujitokeza kupima.

“Watu hawapendi kupima kwasababu ya unyanyapaa katika vituo, pia kutokuwepo kwa usiri, tumepeleka marekebisho ya sheria bungeni ili watu wajipime wenyewe kwahiyo tutagawa vifaa bure ambavyo watu watatumia kujipima maambukizi” amesema Waziri Mwalimu.

Na kuongeza kuwa “awali hakukuwepo sheria inayoruhusu mtu kujipima mwenyewe, haitakuwa kipimo cha mwisho lazima uende kituo cha afya kuthibitisha”

Halikadharika amesema wamekusudia kufanya marekebisho ya sheria ili kuruhusu vijana walio na umri kati ya miaka 10 mpaka 19 kupimwa maambukizi ya Ukimwi tofauti na ilivyo sasa ambapo ni lazima watoto wapate ridhaa ya wazazi.

Waziri Mwalimu amesema katika kila watanzania 100 watu 80 wanauelewa juu ya ugonjwa wa Ukimwi ila changamoto ni kutafsiri uelewa huo kupitia mabadiliko ya tabia katika kujikinga na kutumia tiba na matunzo kwa watu wenye VVU.

Kwaupande wake Naibu waziri wa afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dk. Faustine Ndugulile, amesema kifaa hicho kitakuwa na uwezo wa kugundua kama mtu ana maambukizi ya Ukimwi ndani ya dakika 15 mpaka 20.

Amesema Tanzania siyo nchi ya kwanza kuanza kutumia upimaji huo, na ameeleza kuwa ukubwa wa kifaa hicho kitazidi kidogo kile cha Maralia, hivyo mtu yeyote ataweza kukibeba.

Mwaka 2012 Marekani ilitangaza kuruhusu kuuzwa kwa kifaa cha kupima VVU kwa binadamu ambacho kimetengenezwa mahususi kupima ute na mate.

Serikali yakiri kutokuwa na takwimu za magonjwa yasiyoambukizwa
LIVE: Rais Magufuli akizindua kitabu cha Mkapa ''My Life, My Purpose''