Ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu katika kipindi hiki cha msimu wa mvua za masika Watanzania hasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamehimizwa kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mazingira.

Wito huo umetolewa Desemba 22, 2019 na Mkurugenzi wa Idara ya kinga, wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Dkt. Leonard Subi na kusema pamoja na kwamba mvua ni neema lakini yaweza sababisha madhara ya kiafya kwa binadamu.

“Ni kipindi cha masika sasa na mvua nyingi zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mvua ni neema lakini wakati mwingine ni tatizo katika suala la afya kwa hiyo tuendelee kuzingatia kanuni za afya katika maeneo yetu hasa wakazi wa jiji la Dar es salaam,” amefafanua Dkt. Subi.

Amesema Jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na mlipuko wa homa ya dengue lakini kwa ushirikiano na Serikali hatimaye ugonjwa huo ukadhibitiwa hivyo, wakazi wa jiji hilo waendelee kuhakikisha wanazingatia kanuni za afya.

Aidha Dkt. Subi amesisitiza kuwa watu waendelee kutumia dawa maeneo yaliyozungukwa na maji, kulala kwenye vyandarua, kufukia madimbwi, kuondoa vifuu vya nazi, kutoruhusu kuwepo mazalia ya mbu na utiririshaji wa vinyesi.

“Na tutaomba sheria ichukue mkondo wake kwa yeyote atakayefungulia kinyesi wakati huu wa kipindi cha mvua maana kuna watu wakiona wingu tu tayari na wao wanafungulia chemba za maji machafu na kwa kufanya hivyo wanakuwa wamevunja sheria na huo ni uuaji,” ameongeza Dkt. Subi.

Hata hivyo amewahimizwa wananchi kuendelea kuchemsha maji wanayoyatumia kwa matumizi mbalimbali kwani katika kipindi cha msimu wa mvua baadhi ya vyanzo vya maji huwa vinachafuliwa kwa shughuli za kibinadamu au maporomoko asilia ya maji yanayopita maeneo yasiyo salama.

Dkt. Subi ameongeza kuwa pamoja na kwamba upatikanaji wa maji katika jiji la Dar es Salaam umeimarika hadi kufikia asilimia 85 bado kuna asilimia 15 pungufu hivyo watumie maji safi na salama, kuchemsha maji ya kunywa au kitumia dawa ya chlorine au water guard.

Katika hatua nyingine amewahimiza wananchi wote nchini kuzingatia unawaji wa mikono kwa maji safi na sabuni kabla na baada ya kula na huduma za haja ili kupambana na maradhi sambamba na kutoa wito wa kuhama kwa wale wanaokaa maeneo hatarishi.

Magufuli aagiza vijana 800 wa JKT kuajiriwa
Mabadiliko TEHAMA yahitaji mafunzo ya usalama wa mitandao