Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waishio nje ya nchi  wahakikishe wanashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi yao kwa kushawishi wawekezaji wenye mitaji mikubwa kuja kuwekeza nchini na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Magufuli inaamini kuwa Tanzania itapata maendeleo makubwa ya kiuchumi endapo wananchi wake watatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “Hapa Kazi tu”.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Watanzania waishio nchini China kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo jijini Beijing.

“Tanzania ni nchi nzuri na inaheshimika duniani, nawasihi wote mnaoishi nje muachane kabisa na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa sababu inalitia doa Taifa na adhabu yake katika baadhi ya nchi ni kifo,”amesema Majaliwa

Aidha, Waziri Mkuu amesema China ambayo imefanikiwa kuwa moja kati ya nchi zenye nguvu  kubwa ya kiuchumi duniani, imefika hapo kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na wananchi wake, ambao waliamua kuunga  mkono juhudi za Serikali yao kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wakiwa ndani au nje ya nchi.

Hata hivyo, katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waishio nje ya nchi wajiepushe na vitendo vya uhalifu hasa biashara ya dawa za kulevya ambayo inachafua jina na heshima ya nchi yao kimataifa.

 

LIVE: Rais Magufuli katika hafla ya uwekaji saini mikataba ya ujenzi wa meli mpya
Video: Chadema yapata pigo kuu, Simanzi Monduli