Serikali imewataka Watanzania kuacha kukumbatia tamadumi za kigeni, hususani vijana ambao ndio wamekuwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili kwa kukengeuka na kupotosha Mila na Desturi.

Akizungumza katika uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni, Mila na Desturi ya Mtanzania, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Sanaa,Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo na Makazi Angelina Mabula, amesema serikali imechukua hatua kutokana na mmomonyoko wa maadili kwa kuandaa kitabu, ambacho kitaibua mjadala utakao nyanyua Mila na Desturi.

“Tupende vya kwetu na kuzungumza lugha moja katika kudumisha mila na desturi leo hapa tuna Machifu 94 kutoka kabila zote za Tanzania yote hii ni kuhakikisha asilimia kubwa ya vijana wanatambua umuhimu wa utamaduni wetu,”alisema Mabula.

Aidha Mabula aliwataka wananchi kutambua Rais Samia Suluhu Hassan,amechukuwa jukumu la kutangaza vivutio na mila na desturi za Tanzania,hivyo ipo haja ya kumuunga mkono katika hilo.

Naye Mbunge wa jimbo la Magu Boniventure Kiswaga, amesema ipo haja kila mtanzania kujua chimbuko lake kupitia mila na desturi za kitanzania,ikiwa wengine wamesahau matambiko yao na kupata tabu kutokana na wahusika wa tamaduni hizo kutokudhirikishwa kikamilifu.

“Kutokana na kufutwa kwa mambo ya utawala wa machifu tangu Uhuru,mimi nimeona ipo haja ya kutafuta na kukaa na wadau ili tuweze kupeleka mswaada bungeni ili kuweza kushawishi sheria iliyokuwa ikiwatambua Machifu ilejeshe tena ili kuweza kurudisha mambo ya mila na desturi katika maamuzi ambayo siyo ya kisiasa,”alisema Kiswaga.

“Machifu wanatakiwa kushirikishwa katika masuala ya kidemokrasia ambayo yanahusisha mila na desturi,kiukweli wanapaswa kupewa kipaumbele katika maamuzi ya mambo muhimu ili kusaidia nchi iende mbele katika utamaduni,” amesema.

Nao Umoja wa Machifu Tanzania UMT) umeiomba serikali kuliangalia upya suala la utawala wa machifu, kutokanana kusahaulika katika kuchangia masuala ya maamuzi hususani katika mambo ya mila na desturi.

Akizungumzia katika uzinduzi wa tamasha la utamaduni ,linalo jumuisha makabila zaidi ya 120 kwenye uwanja wa kumbukumbu historia Kisesa, jana wilayani Magu, Mwenyekiti wa Machifu wa Sukuma Land Charles Dotto Itale, machifu hapo awali walikuwa wasimamizi wa mila na desturi kwenye jamii,kwa sasa wamesahaulika na hivyo kusababisha mmomonyoko wa maadili.

RC Makalla: Wanaopangisha Magomeni Kota ni matapeli
Ibada maalumu ya kuwaombea Hayati Magufuli, Mkapa