Watanzania watatu wanadaiwa kuwa miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika shambulizi la kujitoa mhanga lililofanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, Ijumaa, Julai 12, 2019 katika hoteli ya kitalii nchini Somalia.

Kundi hilo lilivamia hoteli Kusini mwa Somalia katika jiji la Kisimayu na kuwaua watu 26 huku likiwajeruhi zaidi ya watu 50.

Waliouawa kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya nchi hiyo ni pamoja na raia wa Tanzania, Kenya, Uingereza, Marekani, Canada na wanasiasa maarufu nchini humo.

Imeelezwa kuwa mmoja wa Watanzania aliyeuawa ni mfanyabiashara mkubwa anayemiliki hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam na Bagamoyo, Mahad A. Nur.

Naibu Waziri wa Afya, Faustin Ndugulile ni mmoja kati ya viongozi wa Serikali waliotoa pole na kuomboleza kifo cha mfanyabiashara huyo kupitia mtandao wa Twitter. Alimtaja Mahad kuwa alikulia Kigamboni jijini Dar es Salaam ambako familia yake inaishi sasa.

Kenya pia imethibitisha kuwa raia wake watatu ni miongoni mwa waliopoteza maisha katika shambulizi hilo.

Aidha, kundi hilo lenye uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda lilimuua mwanasiasa aliyekuwa anatarajia kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Tukio hilo la kigaidi lilidumu kwa takribani saa 14 lakini Jeshi la polisi lilifanikiwa kuwaua magaidi wanne waliokuwa ndani ya hoteli.

“Oparesheni imekwisha. Washambuliaji wanne wameuawa,” Afisa Mwandamizi wa Polisi wa eneo hilo aliiambia Reuters.

“Tumeumizwa sana na tukio hili… waliopoteza maisha ni raia wetu, raia wa kigeni pamoja na wanasiasa wakubwa. Lakini nikwambie tu kuwa tumekasirishwa sana na hatutavumilia,” aliongeza.

Wanamgambo wa Al-Shabaab walivamia hoteli hiyo baada ya kulipua bomu kwenye gari moja na kuzua taharuki.

Wanaotaka Kujiunga Vyuo Vya Elimu ya Juu Watahadharishwa
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 14, 2019

Comments

comments