Polisi wa Mikindu, Kaunti ya Meru nchini Kenya wanachunguza tukio la kuchomwa kwa gari la Mbunge wa Tigania Mashariki, Gichunge Kabeabea lililotokea usiku wa Agosti 6, 2022.

Gari hilo aina ya Toyota Prado, liliteketezwa kwa moto karibu na Daraja la Thiiti, takriban kilomita moja na nusu kutoka mji wa Mikinduri na watu wasiojulikana.

Akiongea mara baada ya tukio hilo, Mbunge Kabeabea amelaumu kisa hicho kwa kumuhusisha mmoja wa wapinzani wake akidai mapema siku hiyo alirushiwa mawe na wahuni walipokuwa wakifanya kampeni mjini Athwana.

“Tulihamia eneo la Mikinduri na niliegesha gari kando ya barabara na kuanza kampeni ya nyumba kwa nyumba iliyolenga makundi madogo ya watu, na nikiwa huko nilitaarifiwa kuwa gari lilikuwa limechomwa nanilipofika nikakuta likiwa limeteketea kwa moto,” amesema Kabeabea.

Amesema, taarifa na kuchomwa moto kwa gari lake alizipata kutoka kwa mwendesha bodaboda ambaye alikuwa akipita alipogundua moto huo, na baadaye Polisi wa eneo hilo wakiongozwa na Mkuu wa polisi wa Tigania Central, Joel Chepkwony walifika eneo la tukio lakini hawakufanya kitu kwani moto ulikuwa mkali.

Hata hivyo, Kabeabea amedai dereva wa gari hilo, Moses Karani pamoja na wasaidizi wawili Kizito Muketha na William Karithi Ruto walitekwa nyara na watu waliodai kuwa ni Polisi, huku msaidizi wake, Lawrence Mutwiri akisema watatu hao waliunganishwa na watu wengine wawili waliokuwa wakimngoja Kabeabea.

Mbunge wa Tigania Mashariki, Gichunge Kabeabea. (Picha na Charles Wanyoro I Nation Media Group)

Kamishna wa Kaunti ya Meru Fred Ndunga amesema Polisi wanajaribu kubaini chanzo cha moto huo kama inahusishwa na watu au ni hitilafu ya kiufundi ili kutoa ripoti iliyo sahihi na kwamba wanatarajia kumhoji Dereva wa gari hilo, Mbunge Kabeabea na baadhi ya wanachama wa timu ya kampeni ya mbunge.

Kenya inatarajia kufanya uchaguzi wake wa Kitaifa hapo kesho Agosti 9, 2022 ambapo Wagombea wote wakiwemo wale wanaochuana kwa karibu Raila Odinga na William Ruto wakiahidi uchaguzi wa amani na kukubali matokeo iwapo hakutakuwa na udanganyifu.

Mashambulizi yauwa 20, Vijiji viwili vikitekwa
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 08, 2022