Mahakama jijini Nairobi nchini Kenya imewahukumu kifo wanaume watatu baada ya kuwakuta na hatia ya kumdhalilisha kwa kumvua nguo mwanamke mmoja kwenye basi la  umma.

Hukumu hiyo ya kifo ilifikiwa na mahakama hiyo baada ya washtakiwa kuongezewa mashtaka ya unyang’anyi na shambulizi la kudhuru mwili.

Tukio hilo lililosababisha wanaume hao kukumbwa na hukumu ya kifo wiki hii, lilirekodiwa na kusambazwa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyoamsha hasira hususan kwa wanawake ambao walifanya maandamano mara kadhaa kupinga na kutaka hatua kali zichukuliwe.

Wanaume hao walishirikiana kumvua nguo mwanamke ndani ya basi la umma kwa kile walichodai wanapinga uvaaji usiozingatia maadili.

Hakimu Mkazi, Andayi amekaririwa na gazeti la Daily Nation kuwa watu hao walionekana kufanya tukio hilo kwa makusudi kwani kipande cha video kinawaonesha wakiwa wanafurahia wanachokifanya huku wakishangilia.

Mamia ya wanawake jijini Nairobi wamekuwa wakishiriki maandamano ya kupinga vitendo wanavyofanyiwa wenzao kwa madai kuwa huvaa sketi fupi. Waandamanaji wanaunga mkono kampeni ya ‘My Dress My Choice’ (vazi langu chaguo langu) ambayo imepata umaarufu pia kwenye mitandao ya kijamii.

Ingawa watu wengi wameonesha kufurahishwa na hukumu hiyo, baadhi ya watu wamepinga wakidai haikuwa ya haki wakiwataka wanawake pia kufikiria kuhusu uvaaji unaozingatia maadili.

Video: Watoto 3 walionusurika ajali ya Lucky Vicent kurejea nchini
Video: Itazame ngoma mpya ya Aslay 'Baby'