Watu watatu waliohusika na utekaji nyara wa zaidi ya wanafunzi 100 katika shule ya sekondari ya Bethel Baptist katika jimbo la Kaduna  nchini Nigeria Julai 5, wamekamatwa na jeshi la polisi nchini humo.

Kwa muujibu wa Msemaji wa Polisi Frank Mba, ameeleza kuwa  waliokamatwa ni miongoni mwa washukiwa 50 wanaoaminiwa kuwa wanachama wa makundi  tofauti yanayowahangaisha watu katika maeneo ya kaskazini  Magharibi na kati mwa Nigeria.

Frank Mba amesema  vikosi vya usalama vinawafuatilia watu wengine 22  ambao ni wanachama wa kundi  ambalo ni sehemu ya utekaji nyara.

Hayo yanajiri wakati mamlaka za majimbo katika maeneo hayo yakitumia makundi ya walinzi kusaidia kudhibiti usalama.

Baadhi ya waathiriwa wameachiliwa, kwa mafungu huku wanafunzi 10 wakiachiwa siku chache zilizopita. Wanafunzi 20 bado wanashikiliwa mateka.

Wazazi wa watoto waliotekwa nyara wameripotiwa kulipa kiasi kikubwa cha pesa kama fidia ili watoto wao waachiliwe lakini madai hayo hayajathibitishwa rasmi.

Utekaji nyara wa wanafunzi hao ulikuwa wa nne katika shule za Kaduna katika miezi michache iliyopita.

Mwandishi wa habari wa ITV afariki dunia
Ujumbe wa Rais Samia katika mkutano wa UN