Wachezaji Djuma Shaban, Khalid Aucho na Bernard Morrison hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara kitakachopambana na Mabingwa wa Soka kutoka Sudan Kusini Zalan FC, kesho Jumamosi (Septemba 17).

Miamba hiyo itakuatana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Young Africans ikiwa na mtaji wa mabao 4-0, walioyapata kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita.

Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amezungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Septemba 16), jijini Dar es salaam akielezea maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo.

Nabi amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo, na kukosekana kwa wachezaji wake watatu hakutaathiri chochote kwenye mipango yake ya kuhakikisha Young Africans inatinga hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Kukosekana kwao kutatoa nafasi kwa wachezaji wengine kuna Joyce Lomalisa atacheza nafasi ya beki akiziba pengo la Djuma,” alisema na kuongeza; “Kutakuwa na mabadiliko mengi kwenye kikosi cha kesho lakini sitafanya mabadiliko yatakayoniumiza nahitaji kuwa na kikosi kizuri ambacho kitaisaidia timu kupata matokeo,”

Wakati huohuo Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema ratiba imekuwa changamoto kwao kutokana na wachezaji wake kushindwa kupata muda wa kupumzika wanacheza michezo mfululizo.

“Ni kweli ratiba ilitolewa mapema lakini hilo haliwezi kunizuia mimi kuzungumza hali halisi iliyopo kwa wachezaji wangu,”

Ikumbukwe kuwa mshindi wa jumla wa mchezo wa kesho kati ya Young Africans dhidi ya Zalan FC atakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Mabingwa wa Ethiopia St George dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal.

Katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Ethiopia St George iliibuka na ushindi wa 1-0, hivyo kujikomboa kwa Al Hilal katika mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mwishoni mwa juma hili kutategemea na matokeo watakaoyapata wakiwa nyumbani nchini Sudan.

Kocha Zalan FC awahofia Fei Toto, Mayele
Mwakinyo apanda viwango vya ubora duniani