Serikali imehimiza watoa huduma za Mawasiliano Nchini, kuzingatia Sheria na Kanuni zilizomo kwenye Leseni katika Utoaji wa huduma husika kwa Wananchi.

Akizindua kikao cha Watoa Huduma za Utangazaji na Maudhui Jijini Dodoma jana Julai 28, 2021, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Jabiri Bakari, amesema baadhi Kanuni za Maidhui na Utangazaji zinafanyiwa maboresho na zinatarajia kuanza hivi karibuni

Dk. Jabiri amesema kuwa TCRA imeboresha utendaji kazi zake kwa kuweka mifumo madhubuti zaidi na imeendelea kutoa ushauri kwa watoa huduma kila mara. Kikao hicho shirikishi pia kilihudhuliwa na watoa huduma za utangazaji na maudhui kutoka vyombo vya habari mbalimbali.

Kikao hicho ambacho kimeratibiwa na TCRA kanda ya kati, kililenga kutoa elimu ya namna bora zaidi katika kufikisha maudhui kwa walaji bila kuwa na migongano baina ya watoa huduma.

Pia kikao kimependekeza wanaochakata maudhui kuangalia namna nzuri zaidi ya kuzuia maudhui yasiyo na staha kwa Jamii ili kuondoa malalamiko ndani ya Jamii. 

Kikao kimependekeza pia vikao kama hivi viwe vinafanywa mara kwa mara ili kuongeza ufahamu zaidi kwa watoa huduma na Mamlaka za Serikali zinazosimamia sekta ya maudhui ya Utangazaji.

Wadau kutoka Azam Media, Multchoice Tanzania limited, Watoa Huduma kwa njia ya Cable, COSOTA na TFF ni baadhi ya washiriki waliohudhuria kikao hicho.

Waziri mkuu mpya wa Haiti atoa ahadi ya uchaguzi wa haraka
Waziri Mhagama afurahishwa na wanufaika mafunzo ya uanagenzi VETA Pwani