Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel na Canada limetoa msaada wa vifaa tiba  vya kufanya uchunguzi wa matatizo ya moyo na vya kutibu magonjwa ya moyo vyenye thamani ya shilingi 81,791,175/= ambavyo vinatumika kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).


Uchunguzi huo pamoja na tiba unafanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo na tiba za magonjwa ya moyo. 


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Stella Mongella alisema vifaa hivyo ambavyo vilitumwa kwa ndege kutoka nchini Israel vitafanya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na mapafu kwa watoto 10 , kuziba matundu ya moyo kwa watoto 12 na matibabu ya dharura kwa watoto wachanga watatu. 


“Vifaa tulivyovipokea ni vya kuziba matundu 12, kufanya uchunguzi 10 na vifaa vitatu vyenye puto maalum ambalo linatumika kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura kwa watoto wachanga wenye shida ya moyo ambao mishipa yao mikubwa ya moyo imejigeuza,” 

“Mshipa mkubwa wa moyo unaotakiwa kutokea chumba cha kulia umetokea kushoto na mshipa wa chumba cha kushoto umetokea kulia,”
“Watoto wachanga hawa huwa wanaumwa sana siku za mwanzo na wanahitaji matibabu maalum ya kuwaongezea ukubwa wa tundu ambalo liko katikati ya moyo kwenye vyumba vya juu vya moyo, kwa kumuongezea hilo tundu kunampa unaafuu wakati anasubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo”, alisema Dkt. Stella. 


Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliwashukuru SACH  Israel na SACH Canada ambao wametoa msaada wa vifaa hivyo ambavyo wanavitumia kufanya uchunguzi wa vyumba vya moyo, mishipa ya damu inayotoka na inayoingia kwenye moyo pamoja na kupima msukumo wa damu kwenye mapafu na  kwa watoto ambao mioyo yao ina matundu wanayaziba.

Haji Manara kuhama Tanzania
Manara: Msimu huu ni shangwe tu