Taharuki imeibuka katika Kijiji cha Halambo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe baada ya watu 25 kufikishwa katika hospitali ya wilaya hiyo kwa madai ya kuugua baada ya kunywa pombe ya kienyeji.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi Digital inadaiwa watu hao walikunywa pombe hiyo sehemu moja ambapo baadae walianza kuumwa tumbo na kuhara na walipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati ya kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Halambo, Lazima Mwambani amesema siku ya tukio hilo Ijumaa Juni 2, 2023 kulikuwa na msiba kijijini hapo ambapo baada ya mazishi watu walienda kunywa pombe kilabuni hapo.

“Tukio hilo lilitokea Juni 2 mwaka huu na idadi ya walioathirika ni watu 31 ambapo baadhi yao walipata madhara siku hiyohiyo lakini wengine walianza kuumwa siku iliyofuata” amesema Mwambani.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Dk Nelson Mponjoli amesema aliwapokea watu 25 ambao walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani kwao.

“Siwezi kuthibitisha kama walikunywa kinywaji chenye sumu ninachoweza kusema watu 25 walifikishwa hospitalini wakiwa wanasumbiliwa na kuhara na tumbo kuuma, hata hivyo hali zao hazikuwa mbaya walitibiwa na kuruhusiwa kurudi,” amesema Mponjoli

Aidha, Mwenyekiti wa kijiji hicho amesema mpishi wa pombe hiyo anadaiwa kukimbia mara baada ya kusikia watu wanaumwa, lakini mume wake anashikiliwa na Polisi.

Pia, kati ya watu 31 waliokumbwa na madhara hayo inasemekana 25 tu ndio waliofikishwa hospitali ya wilaya huku wengine sita wakitibiwa sehemu nyingine.

Rais Samia awaalika Yanga Ikulu
Chanzo cha ajali ya tren iliyoua watu 300