Zaidi ya watu 50 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa baada ya mtu mmoja kufyatua risasi hovyo kwenye tamasha la muziki Las Vegas, Marekani.

Vifo hivyo vimetokea leo baada ya mzee mwenye umri wa miaka 64 kufyatua risasi hovyo kutoka katika ghorofa ya 32 ya hoteli ya Mandalay Bay akizielekeza katika tamasha la wazi la muziki.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mshambuliaji huyo aliyetambulika kuwa ni mkazi  wa eneo hilo aliuawa kwa risasi na maafisa wa jeshi la polisi.

Jeshi la polisi linamsaka mtu aliyekuwa na mshambuliaji huyo muda mfupi kabla ya kufanya mauaji hayo.

Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Joe Lombardo ameviambia vyombo vya habari kuwa jeshi hilo pia linamsaka mwanamke mmoja mwenye asili ya bara la Asia anayefahamika kwa jina la Marilou Danely.

Hata hivyo, Lombardo alisema kuwa bado hawajapata idadi kamili ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.

Msemaji wa hospitali ya eneo hilo ambayo pia ilipokea majeruhi alisema kuwa zaidi ya majeruhi 14 walikuwa katika hali mbaya.

Tamasha hilo la muziki lilikuwa likifanyika katika hoteli kadhaa kwenye eneo la Las Vegas tangu Ijumaa ya wiki iliyopita.

Kichapo cha Tanzanite chamgusa Mwakyembe
Airtel yazindua ofa ikisherehekea wiki ya huduma kwa wateja