Watu watano wamejeruhiwa baada ya basi lililokuwa na zaidi ya abiria arobaini kupinduka katika eneo la Cheyo Manispaa ya Tabora.

Basi hilo kampuni ya Abood ambalo linafanya safari za Tabora-Dar es salaam limepata ajali leo Jumapili Januari 9, 2022 muda mfupi baada ya kutoka mjini Tabora.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk Yahaya Nawanda ameeleza kuwa abiria watano waliopata majeraha wamepelekwa kupata matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.

Amesema abiria wengine ambao hawakupata majeraha, wameendelea na safari kwa kutumia basi la kampuni ya Kisbo.

“Utaratibu umefanywa abiria kuendelea na safari na waliojeruhiwa kupelekwa Kitete kwa matibabu,” alisema Dkt Nawanda.

Shuhuda wa ajali hiyo, Sadick Yassin mkazi wa Cheyo amesema aliona basi hilo likipita pembeni ya barabara sehemu ambayo mabasi hayapiti na kupinduka.

“Dereva alipita pembeni ya barabara jirani na reli na kushindwa kulimudu ambapo lilipinduka.” Alisema Shuhuda.

Mmoja wa Polisi aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa vile sio msemaji, amesema chanzo ni uzembe wa dereva wa basi kupita sehemu isiyo rasmi kwa mabasi.

Dereva wa basi hilo ambaye jina lake bado halijafahamika amedaiwa kukimbia baada ya ajali kutokea.

Akamatwa akipata chanjo ya Corona mara ya 11
Umeme uwake kabla ya Juni- Mavunde