Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na ubunifu ili kuboresha huduma na kuongeza mapato.

Ameyasema hayo mjini Shinyanga alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi hizo ambapo amesema kuwa Serikali itaendelea kuajiri watumishi wenye weledi na uzoefu wa kutosha katika Taasisi hizo hivyo kazi kubwa ni kuwapa ushirikiano na kufanyakazi kwa malengo yanayopimika.

“Tumejipanga kumaliza changamoto ya uhaba wa wafanya kazi hasa kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Wakala wa Majengo Nchini (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) hivyo ongezeni ubunifu ili kuwe na uwiano kati ya wafanya kazi na tija inayozalishwa katika Taasisi zenu”, amesema kwandikwa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi, Mibara Ndirimbi amemhakikishia kuwa licha ya upungufu wa wafanya kazi barabara zote kuu na za mikoa zinapitika wakati wote wa mwaka.

Naye Kaimu Meneja wa TBA Shinyanga Mkadiriaji Majenzi, Emmanuel Julias amesema ofisi yake inasimamia ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia nafaka vyenye uwezo wa kutunza tani zaidi ya elfu 20 hivyo kukamilika kwa mradi huo licha ya kuongeza mapato pia kutaongeza uzoefu kwa taasisi hiyo na hivyo kuomba wadau wengi mkoani humo kuitumia.

 

Vyama vya upinzani vyaungana kuhusu kesi ya Mbowe na Matiko
LA Galaxy kuachana na Ashley Cole, Ibrahimovic apeta