Wanasiasa, wanaharakati pamoja na asasi za kiraia nchini Tunisia wametangaza kufanya maandamano makubwa mbele ya Ikulu ya nchi hiyo, kupinga ziara ya Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.

Makundi hayo yametangaza maandamano hayo wakidai kuwa Mwana wa Mfalme hakaribishwi kutokana na tuhuma za kuamuru mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul, Uturuki.

Msemaji wa Serikali ya Tunisia, Saida Qarash amethibitisha kuwa Mwana wa Mfalme, Mohammed atazulu nchi hiyo Novemba 27 mwaka huu.

Qarash amesema kuwa nchi hiyo inalaani vikali mauaji ya Khashoggi na msimamo wake ni kuvitaka vyombo husika kuweka ukweli hadharani.

Aidha, mwanaharakati maarufu nchini humo, Tarek kahlawi amesema kuwa mamia ya wananchi watakusanyika mbele ya Ikulu ya Carthage, kupinga ujio wa Prince Mohammed.

“Ni aibu kuona kuwa Tunisia, ambayo imeshuhudia mabadiliko ya kidemokrasia na mapinduzi dhidi ya udikteta, itampokea mhalifu ambaye mikono yake imejaa damu ya wananchi wa Saudi na Yemeni,” Al Jazeera inamkariri Kahlawi.

Mwana wa Mfalme aliwasili Abu Dhabi Alhamisi wiki hii na anatarajia kuendelea na ziara yake akipitia Bahrain na Misri.

Aidha, atahudhuria mkutano wa G20 utakaofanyika nchini Argentina mwishoni mwa mwezi huu, ambako atakutana na viongozi mbalimbali wa dunia akiwemo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ambaye amekuwa akimtuhumu kuwa alihusika kwa namna moja au nyingine na mauaji ya Kashoggi.

Hivi karibuni, Rais wa Marekani, Donald Trump alieleza kuwa ripoti ya CIA dhidi ya mauaji hayo haikuhitimisha kwa kumtaja Mwana wa Mfalme kuamuru mauaji ya Khashoggi kama inavyodaiwa na wengi.

Video: Katibu Tawala wilaya ya Kinondoni awafunda wahitimu wa ufundi Cherehani
Video: Diwani Urio aahidi neema kwa wahitimu wa ufundi Cherehani, Kunduchi Jijini Dar