Jeshi la Polisi Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, linawashikilia wauguzi saba kwa tuhuma za wizi wa dawa na kudaiwa kuwauzia wagonjwa nyakati za usiku.

Hayo yameibainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Anderson Msumba wakat akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kwa muda mrefu amekuwa akipokea malalamiko ya wagonjwa kuuziwa dawa usiku wa manane na wauguzi kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Amesema, baada ya kupokea malalamiko hayo walifanya kazi kwa kushirikiana na maafisa kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa )TAKUKURU) ambapo walifanya ukaguzi wa kushtukiza katika hospitali februari 24.

Aidha, amesema katika ukaguzi uliofanyika usiku kwa wauguzi wa zamu siku hiyo saba walikutwa na dawa kwenye mikoba yao ya mikononi pamoja na drip za maji.

“Dawa wanazouziwa wagonjwa na wauguzi hawa hatujui ubora wake na wapi wanazitoa kwasababu biashara hiyo wamekuwa wakiifanya usiku wa manane katika wodi na hii inasababisha hospitali kukosa mapato yake vile inavyotakiwa” alisema Msumba .

Hata hivyo, baada ya tukio hilo alifanya kikao kazi na wauguzi wa hospitali hiyo na kukubaliana kutumia geti moja la wagonjwa wa nje kwasababu awali yalikuwa yakitumika mageti mawili na kukubaliana kila siku msimamizi wa wodi kutoa taarifa yake ya kila siku.

Pia Msumba amesema uchunguzi wa jeshi la polisi utakapo kamilika watachukua hatua zingine za kiutumishi huku akiwataka watumishi wengine wa kada ya afya kuacha tabia ya kuuza dawa.

Wanne mbaroni wakijifanya wachezaji wa Coastal
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 12, 2023