Watumishi watano wa hospitali ya Butimba wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, wamesimamishwa kazi baada ya mzazi kujifungulia kwenye beseni watoto mapacha ambao walifariki muda mfupi baadae, kwa kile kilichodaiwa kukosa huduma wakati akijaribu kujifungua hospitalini humo.

Akielezea tukio hilo, mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Suzan John mwenye umri wa miaka 27, alidai kuwa alianza kusikia uchungu na kuomba msaada kutoka kwa madaktari na wahudumu wa afya waliokuwa hospitalini humo bila mafanikio.

“Kwenye beseni mle watoto vitovu vilikuwa vinachungulia. Nikaita manesi, wakawa wanakuja tu wananichungulia wanarudi. Akaja Nesi mmoja mwanafunzi, akakata kitovu akawaweka kwenye nguo, wakawa wamefariki,” Bi. Suzan alieleza kwa uchungu huku akilia.

Baadhi ya mashuhuda walieleza kuwa walifanya jitihada za kuwaita wahudumu lakini waliishia kupewa majibu ‘mabovu’ yaliyowakatisha tamaa.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga alitangaza uamuzi wa kuwasimamisha kazi waganga na wauguzi waliokuwa zamu.

“Hatuna sababu ya kuendelea na watu wa aina hiyo katika hospitali yetu ya serikali. Wakatafute kazi huko kwingine,” alisema Konisaga.

Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo ameunda kamati ya kuchunguza tukio hilo, itakayoongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Onesmo Lokendelya.

Magufuli ahamishia kasi ya ujenzi Afrika Mashariki, asema Wananchi hawahitaji ‘mavyama’
Wassira amchana January Makamba