Wakati waumini wa dini ya kikristo wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka leo Jumapili Aprili 17, huko Mbalizi Mbeya, baadhi ya waumini wa usharika wa Mbalizi wamemzuia mchungaji wao, Atupele Mlawa kuingia kanisani na kusababisha kuvunjika kwa ibada.

Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi mkoani humo limefika kanisani hapo na kukamata baadhi ya viongozi wa kanisa hilo, Wakati mgogoro ukizidi kufukuta kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei amesema baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa vurugu aliwatuma askari wake kwenda kumaliza mzozo.

Viongozi wanaotajwa kukamatwa na Polisi ni pamoja na Askofu wa dayosisi ya Mbeya Magharibi, Judith Kajela, Mchungaji Atupele Mlawa na Mchungaji Lusajo Sanga.

Taarifa zaidi zimesema waumini wanaompinga Mchungaji Mlawa, wanamtaka Mchungaji Lusajo Sanga aliyechaguliwa hivi karibuni kwenye uchaguzi uliofanyika Machi 22 chini ya Kiongozi wa Kanisa hilo nchini, Dk Fredrick Shoo.

Hata hivyo taarifa zaidi zinasema Mgogoro huo sasa umefika mahakamani wakati Msajili wa Jumuiya, Emmanuel Kihampa akibariki kuondolewa kwa Askofu Edward Mwaikali wa Dayosisi ya Konde.

Taarifa kuhusu kesi hiyo zinaeleza kuwa Askofu Mwaikali amefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya dhidi ya Baraza la Wadhamini KKKT na watu wengine 28, akiwamo Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo akiwa ni mdaiwa wa pili katika shauri hilo. Katika orodha ya walioshtakiwa, wamo wachungaji 11, akiwamo Askofu mteule wa Dayosisi ya Konde, Geofrey Mwakihaba, Dk Mechack Njinga aliyechaguliwa msaidizi wa Askofu na Jackson Mwakibasi aliyekuwa mwenyekiti wa uchaguzi.

Mara zote, Askofu Mwaikali na baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wamedai Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Machi 22, 2022 na kumuondoa Askofu Mwaikali ni batili na ulikiuka Katiba ya Konde.

Kutokana na hatua hiyo, uongozi wa KKKT umeuomba uongozi wa Mkoa wa Mbeya kuwapa ushirikiano viongozi wapya wa dayosisi hiyo ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo.

Hata hivyo, alipoulizwa juzi, Katibu Mkuu wa KKKT, Mhandisi Robert Kitundu alisema hana taarifa ya kufunguliwa kwa kesi hiyo.

Chinga aliyenyang'anywa ndizi asherehekea Pasaka ya viwango vya juu
Faida za Parachichi mwilini