Wavuvi katika bwawa la Mtera kambi ya Mwakibwera wamelalamikia watumishi wanaokusanya mapato wa halmashauri ya wilaya wa Mpwapwa kwa kuvamia na kuvunja mitumbwi yao wakati wamelipia leseni ya kufanya biashara hiyo.

Wavuvi hao wamewaambia waandishi wa habari kuwa kwa nyakati tofauti wakusanya mapato wamevunja mitumbwi 17 na kuwasababishia hasara ya Tsh. milioni 5.1.

Imeelezwa kuwa kutokana na kuvunjwa kwa mitumbwi hiyo familia zao zimefanywa kuwa masikini zaidi kutokana na kukosa kipato kilichokuwa kikitokana na shughuli za uvuvi katika bwawa hilo la Mtera.

Mvuvi Joseph Mgeni amesema kuwa watumishi sita walifika na kuvunja mitumbwi hiyo kwa kutumia shoka na kueleza kuwa anasikitika kwa kitendo hicho kwani hakuna hata mvuvi mmoja aliyemiliki mtumwi bila kulipia leseni.

Mvuvi Hussein Mkwizu yeye ametoa ombi kwa watumishi hao kuwa na utaratibu kabla ya kuchukua hatua kukaa pamoja na wavuvi hao na kuwapatia elimu ya kuwa na leseni.

Diwani wa kata ya Mtera, Amon Kodi amesema taarifa ya kuvunjiwa mitumbwi hiyo alipatiwa na wananchi kitendo ambacho amedai ni kinyume na sheria.

“Kisheria, bwana – samaki haruhusiwi kuvunja mitumbwi bali anatakiwa kukamata chombo na kikikaa siku 90 baada ya hapo anatakiwa kwenda Mahakamani kwaajili ya kuomba kuteketeza kwa kuchoma moto mitumbwi au nyavu” amesema Diwani Kodi.

Hata hivyo Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Daud Sweha ameahidi kufuatilia na kufanyia kazi suala hilo.

Mwili wa mwanahabari aliyefariki kusafirishwa leo
TCRA kuwasaka waliosajiliana laini za simu