Ujumbe wa wawekezaji zaidi ya 30 kutoka Afrika ya Kusini, wamekutana na Wizara ya Madini pamoja na Taasisi zake kwa lengo la kupata uelewa wa mazingira ya uwekezaji nchini.

Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga amewashauri wawekezaji hao kuwekeza kwenye shughuli za Madini ikiwemo Uchimbaji wa Madini,  Uongezaji Thamani Madini na uuzaji wa vifaa vya shughuli za madini.

Dkt. Mwanga amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na Madini ya aina mbalimbali yakiwemo Madini ya kimkakati ambayo kwa sasa dunia inayahitaji kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia.

Aidha, amewapongeza wawekezaji hao kwa kufika nchini ili kupata maelezo na kujifunza mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na amewaahidi kupata ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha shughuli za uwekezaji nchini.

Nayo, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetumia fursa hiyo kuwasilisha mada juu ya uwepo wa Madini na kiwango cha Madini kilichopo katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na jiografia ya Tanzania.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo Roelof Tonder amesema Afrika  Kusini imeanza shughuli za Madini miaka mingi iliyopita hivyo, imefarijika kuona Tanzania imefanya marekebisho makubwa kwenye Sheria ya Madini ambayo yanalenga kuinufaisha nchi pamoja na Wananchi.

Haya yanajiri kufuatia ziara  ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  aliyoifanya hivi karibuni nchini Afrika Kusini.

Uganda yashikilia msimamo wake, yasema haipangiwi
Wasanii wa Bongo kwenye Playlist ya Kamala Harris wa Marekani