Wawekezaji kumi wanaomiliki makampuni mbalimbali ya biashara nchini Rwanda wameunda Kampuni moja kwa lengo la kuwekeza mkoani Kagera katika Sekta ya ufugaji wa kisasa.

Wawekezaji hao wenye lengo la kufungua kiwanda cha kusindika nyama mkoani humo, leo, Septemba 11, 2019 wamefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ili kumweleza nia yao.

William Kawamala, kiongozi wa wawekezaji hao kutoka nchini Rwanda amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wapo tayari kuwekeza katika sekta ya ufugaji  wa kisasa wa ng’ombe kwa kushirikiana na Kampuni za  Ranchi za Taifa (NARCO) baada ya kupata fursa hiyo katika Wiki ya Uwekezaji Kagera iliyofanyika Agosti 12 hadi 17, 2019.

“Baada ya kushiriki Wiki ya Uwekezaji Kagera tulivutiwa kuwekeza katika Sekta ya ufugaji, na tuliporudi kwetu nchini Rwanda tilikaa pamoja na kukubaliana tujiunge kwa pamoja wafanyabiashara kumi ili kuanza uwekezaji mara moja, ndiyo maana tupo hapa ili kuanza hatua za awali. Pia, tumekuja kuona maeneo ya kufugia na kuweka kiwanda,”  Kawamala amemueleza Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa Gaguti amesema kuwa Serikali ya Mkoa huo iko tayari kuwapa ushirikiano. Amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Prof. Philemon Wambula pamoja na baadhi ya wataalam kutoka Sekretarieti ya mkoa  kuwaonesha maeneo yaliyotengwa pamoja na taratibu  za kusajili kampuni na kuanza uwekezaji zianze mara moja.

“Baada ya Wiki ya Uwekezaji mwitikio umekuwa mkubwa sana wa wawekezaji kuja kwetu kuchangamkia fursa zilizopo Kagera na sisi tumejipanga tunawapokea na kuwaelekeza taratibu za uwekezaji, lakini jukumu letu ni kuhakikisha fursa zote ambazo wawekezaji wameziona wanazitumia katika uwekezaji ili kukuza uchumi wa mkoa wetu,” amesema Mkuu huyo wa mkoa.

Profesa Philemon Wambura, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO) ameeleza kuwa mkoa wa Kagera bado una fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya mifugo hasa katika viwanda vya kusindika nyama na maziwa pia uwekezaji katika malisho ya mifugo, nakuongeza kuwa NARCO bado inayo maeneo makubwa ya kuwekeza.

Ujumbe wa Makonda, Jokate baada ya Nape kumuomba msamaha Rais Magufuli
Mwili wa Mugabe kuwasili Zimbabwe leo, mazishi jumapili