Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davuto Glu wameongoza ujio na mapokezi ya Wawekezaji wa makampuni saba makubwa ya nchini Uturuki ambao wamewasili kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa Viwanda.

Wawekezaji hao wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwepo viwanda, Kilimo na Sekta ya umeme, ambapo mikoa ya Dodoma na Simiyu imepewa kipaumbele na wawekezaji hao ambao wataanza zoezi hilo la ujenzi wa viwanda ifikapo mwezi Juni mwaka 2019.

Akizungumza katika kikao cha pamoja cha wawekezaji hao na Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki, Prof. Elizabeth Kiondo amesema kuwa hatua ya wawekezaji hao kuonyesha nia ya kuwekeza nchini inatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo pamoja na juhudi za kuwahamasisha.

“Ndugu zangu Wawekezaji hawa wamekuja wakati muafaka kabisa wakati ambao Serikali yetu inahimiza uchumi wa viwanda, pia ni kwa sababu Serikali yetu imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, lakini pia tumekuwa tukiwahamasisha waje kuwekeza hapa kwetu Tanzania,” Amesema Prof. Kiondo.

Aidha, amesema kuwa bado wana kazi kubwa ya kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini Uturuki kuja Tanzania kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na hivyo ujio wao ni mwanzo tu wa wawekezaji wengine kuja kuangalia fursa na mazingira yaliyopo.

Naye Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania, Ali Davuto Glu amesema kuwa Tanzania inaelekea kufikia malengo makubwa ya kiuchumi hali inayoungwa mkono na Serikali ya Uturuki na kuamua kuwahamasisha wawekezaji wa nchini humo kuja kuwekeza Tanzania.

Kwa upende wake Mkurugenzi wa uhamasishaji na Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, John Mnali amezitaka taasisi zinazohusiana na maeneo ya uwekezaji kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ili kurahisisha kazi hiyo kufanywa kwa wakati.

Bosi wa kampuni ya Nissan akamatwa kwa ufisadi
Florentino Perez kumsajili Pedrinho

Comments

comments