Wawekezaji zaidi ya 140 kutoka Italia wamewekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania yenye thamani ya shilingi bilioni 5 inayotoa ajira kwa watanzania zaidi ya 4000.


Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Wizara ya Madini, Prof. Shukrani Manya alipokuwa akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika leo Jijini Roma, Italia.


“Jukwa hili tunataka liendelee kuwa sababu ya kuchagiza uwekezaji mwingine kutoka Italia kwa kutumia teknolojia waliyonayo, kwa kutumia utalaamu walionao wa designing na sasa waone kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na Tanzania inaendelea kuweka mazingia wezeshe ya kukuza sekta ya uwekezaji na biashara,” Amesema Prof. Manya.


Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mahmoud Thabiti Kombo amesema kuwa kufanyika kwa kongamano hilo la biashara na uwekezaji lengo lake kubwa ni kuwavutia wafanyabiashara na wewekezaji wa sekta mbalimbali kutoka Italia kuwekeza zaidi Tanzania.


“Mwitukio ni mkubwa na tumeitikiwa na jumuiya za kibiashara na wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka nchi zote mbili wameshiriki katika kongamano hili,” Amesema Balozi Kombo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.


Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki katika jukwaa hilo kuwa CRDB ipo tayari kutoa mikopo kwa watakao kuwa tayari kuwekeza Tanzania.


Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.


Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Taifa ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Kituo cha daladala Buguruni kurejea tena
Chanjo za Janssen zawasili nchini