Jumuiya ya Zanzibar waishio Marekani (ZADIA) wameandamana hadi katika ikulu ya Marekani (White House) kushinikiza nchi hiyo kuingilia kati mzozo wa kisiasa unaendelea kufuatia tangazo la kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25.

Wananchi hao wameandamana wakiwa wamebeba mabango mbalimbali yenye jumbe zilizolenga kumtaka Rais Barack Obama kuingilia kati na kulinda demokrasia Zanzibar.

Bango

Mwenyekiti wa ZADIA, Omar Haj Ali alisema kuwa tayari walikuwa wamemuandikia barua rais Obama kumtaka aingilie kati sio tu kwa maneno bali kwa vitendo ili kuhakikisha matakwa ya demokrasia na uamuzi wa wananchi unaheshimiwa.

Alisema kuwa wana imani na rais Obama kuwa atayafanyia kazi maombi yao na kwamba wamemkumbusha ahadi yake ya kuhakikisha anasimamia demokrasia katika bara la Afrika.

“Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu, rais Obama alisema kuwa pale ambapo wananchi hawawezi kutekeleza haki zao basi ulimwengu una jukumu la kukemea na Marekani itafanya hivyo, hata kama wakati mwingine itakuwa inauma,” alisema Ali.

Alisema kuwa kwa kuwa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulikuwa wa kwanza kutoa taarifa kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru na haki, ana imani kuwa Obama atafanyia kazi malalamiko ya Jumuiya hiyo na kwamba atachukua hatua kulinda demokrasia Zanzibar.

 

Julius Mtatiro afunga mjadala wa Ubunge wa Segerea
Waziri Aliyekumbwa Na Ufisadi Wa Kununua Kalamu Moja Sh 200,000 Achukua Hatua