Wazazi wa wanafunzi wa shule ya Chengdu nchini China wameandamana na kuvamia eneo la shule hiyo kwa madai kuwa wamebaini watoto wao hulishwa vyakula vilivyooza na vilivyoisha muda wake wakiwa shuleni hapo.

Kwa mujibu wa The Guardian, wazazi hao waliofurika nje ya jengo la shule hiyo walipambana na askari waliokuwa wakijaribu kuwatawanya kwa kile kilichodaiwa kuwa walitaka kufanya uharibifu kwa hasira.

Polisi wa eneo la Chengdu wametoa taarifa kwa umma na kueleza kuwa wanawashikilia wazazi 12 wakiwahusisha na vurugu zilizofanyika katika shule hiyo.

Wazazi wa shule hiyo wanadaiwa kuibua suala hilo hatari kwa afya baada ya kufika katika mgahawa wa shule walipoenda kuwatembelea watoto wao, BBC imeripoti. Wanadai kuwa walipoona dalili hizo waliingia hadi jikoni na ndipo walipojiridhisha kuwa vyakula havikuwa vinafaa kwa matumizi ya binadamu.

Picha zinazosadikika kuwa ni za vyakula kutoka katika shule hiyo zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii ya China. Gazeti la The Guardian limeikariri tweet ya mmoja wa wazazi hao ikieleza kuwa uchunguzi wa daktari umebaini kuwa mtoto wake alikuwa akila vyakula vilivyooza.

Hashtag ‘ChengduNo7’ iliyotumika kuzungumzia tukio hilo imeangaliwa zaidi ya mara milioni 200, lakini sasa Serikali imedhibiti uangaliaji wa picha hizo kwenye mitandao ya China kuepuka kuongeza taharuki.

Hata hivyo, baadhi ya video zinazoonesha maandamano ya wazazi nje ya shule hiyo zimewekwa YouTube tayari.

Uongozi wa shule hiyo umeomba radhi kwa umma kutokana na hali hiyo na kuahidi kusimamisha utoaji wa huduma ya vyakula kutoka kwa mzabuni aliyekuwa anatoa huduma hiyo.

Mkurugenzi wa idara ya afya ya eneo hilo, Yuan Xiaoling ameandika katika mtandao wa Weibo kuwa baada ya kupima sampuli walizozichukua katika mgahawa huo, wamebaini hakuna dalili zozote za magonjwa yatokanayo na chakula kilichoharibika.

“Vituo vyetu viwili vimefanya uchunguzi wa sampuli,  vimechukua sampuli ya vyakula vilivyokuwa vimebaki kwenye mgahawa wa shule na matokeo yake ni kwamba hakukuwa na dalili hasi,” alisema Yuan Xiaoling.

Pacquiao apata mpinzani mpya, ni Spence Jr. aliyeshinda leo mbele yake
Video: Mrithi wa Maalim Seif huyu hapa, Magufuli awafukuza TBA, Magereza 'site'