Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, imekataza Mamlaka ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kuruhusu watu au taasisi zisizo na mamlaka kisheria kuwaamuru kupima sampuli za vinasaba (DNA).

Dk. Ndugulile ameitaka mamlaka hiyo kutoa elimu kwa jamii kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, ili kuepuka watu au taasisi kutoa maagizo juu kwa mamlaka hiyo kinyume cha sheria na taratibu.

“Tusiamini kila mtu anajua utaratibu. Tunaweza sasa kuja kuvumbua mambo ambayo hayapo. Si kila mtu anaweza kuamrisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua vipimo vya DNA, si hivyo kuna taratibu zake,” alisema.

Dk. Ndugulile aliitaka taasisi hiyo kuwa na mkaguzi wa kimataifa wa ubora wa sampuli wanazopima, ili zikubalike kitaifa na kimataifa.

“Lazima muwe na mkaguzi wa kimataifa wa kuthibitisha kile mlichopima kwa sababu taasisi hii ina majukumu ya kisheria ya kuamua ukweli kuhusu sampuli iliyopimwa. Mkisema huu ni unga wa mahindi ilhali tunaona ni dawa za kulevya hatuwezi kupinga,” alisema.

Dk. Ndugulile amesema katika siku za karibuni suala la kupima vinasaba limezungumziwa sana hali ambayo imezua mkanganyiko kwa jamii, hivyo kuitaka mamlaka hiyo kutimiza wajibu wa kutoa elimu na kufikia maamuzi hayo.

Ndalichako aagiza Nacte na TCU kuvifungia vyuo visivyokidhi vigezo
Ummy Mwalimu amkosoa Goodluck Mlinga