Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijini (RUWASA) Wilaya ya Karagwe, Mhandisi Magai Kakuru kwa kushindwa kusimamia miradi ya Maji inayoendelea kutekelezwa Wilayani humo.

Agizo hilo la kusimamishwa kazi limetolewa na Waziri Aweso Septemba 11, 2022 baada ya kutoridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Chanika/Omululama katika ukaguzi alioufanya akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa.

Amesema, “Mhandisi huyu anajitahidi kufanya kazi lakini haiendani na kasi inayohitajika kwahiyo ataenda kusaidia kwenye kazi nyingi, hapa karagwe nitaleta Meneja Mwingine anayeendana na kasi tunayoitaka.”

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Kushoto), akiongea mbele ya waandishi wa Habari. Anayefuata ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa.

Waziri Aweso ameongeza kuwa, awali akiwa Wilaya karagwe alitoa maelekezo kuhusu miradi ya maji, lakini hadi kufikia ukaguzi wa miradi hiyo, amegundua wakandarasi hawapo makini na fedha za miradi.

Kufuatia hali hiyo, Aweso ameagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Vijiji vinane Wilayani Karagwe aondolewe na mchakato wa kupata Mkandarasi mwenye uwezo atakayetekeleza miradi ya maji ndani ya muda.

Aidha, Waziri Aweso amesema “Serikali haitamvumilia wala kumbembeleza Mhandisi yeyote atakayeshindwa kusimamia miradi ya maji faraja ya Mhandisi wa Maji ni kuona Wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.”

Ukaguzi wa utekelezaji wa Mradi wa maji ukiendelea.

Katika hatua nyingine, Waziri aweso pia amesema hatakubali kuona Meneja wa Maji wa Mkoa ana zaidi ya shilingi Bilioni 9 kwenye akaunti lakini wananchi wanaendelea kuhangaika na kero ya Maji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema kiu ya Wananchi wa wilaya ya karagwe ni kuona miradi ya maji inakamilika na kuanza kutoa huduma.

Kocha Simba SC aihofia Nyasa Big Bullet Kwa Mkapa
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 12, 2022