Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile ametoa onyo kwa watoa huduma za mawasiliano nchini kuacha tabia ya kuvujisha taarifa binafsi za wateja.

Ndugulile amebainisha hayo wakati akizungumza na watoa huduma za mawasiliano katika hafla ya kutia saini Mkataba baina yao na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kupeleka huduma za mawasiliano katika vijiji 173 vilivyo katika mikoa 16 nchini.

“Niwaombe sana makampuni ya simu, someni vizuri sheria, vyombo vya dola ndivyo vinavyoruhusiwa kupata taarifa binafsi za mteja kwa malengo mahsusi na sio vinginevyo”, alisisitiza Ndugulile

Ameongeza kuwa suala hilo atalisimamia kwa umuhimu wake na kampuni ya simu itakayotolewa malalamiko na wananchi kwa kuvujisha taarifa zao, hatua kali zitachukuliwa dhidi ya kampuni husika.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Andrea Kundo ametoa rai kwa watoa huduma za mawasiliano kuwa watafiti na wabunifu kwa kufanya uwekezaji kwa kutumia teknolojia nyepesi itakayowezesha mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.

JPM kuzindua shamba la miti
Wanajeshi waondoka nyumbani kwa Bobi Wine