Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amefungua milango kwa wakandarasi wa visima ambapo ameelekeza wapewe fursa za kuchimba visima badala ya kutumia Wakala wa Uchimbaji pekee ambao kila mwaka wamekuwa wakishindwa kutimiza malengo ya visima ambavyo wizara imekuwa ikipanga.

Waziri Aweso ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 28, jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na wakandarasi wa uchimbaji visima na watafiti wa maji chini ya ardhi katika warsha iliyowakutanisha Wizara ya Maji na wadau hao kuhusu miongozo ya utafiti, uchimbaji visima na changamoto zao ili kuboresha eneo hilo katika muktadha wa mageuzi ya Sekta ya Maji.

Amesema katika msingi wa kukidhi dhamira ya Rais Rais Samia Suluhu Hassan kuona Watanzania wakipata maji safi, salama na yenye kutosheleza ameahidi kufanya mageuzi makubwa kwa Wakala wa Serikali wa Uchimbaji Visima (DDCA).

“Kwa mfano mwaka huu tuna mpango wa kuchimba visima zaidi ya 1,000 na niwaambie tu Wakala wa Uchimbaji toeni fursa kwa hawa wachimbaji, haiwezekani mnachimba kisima mwezi mzima bila sababu ya msingi, wapeni hawa wachimbaji muone kama hawatochimba kwa siku moja,” amesema Aweso.

Pamoja na mambo mengine, amewaahidi wachimbaji hao kushughulikia changamoto zinazowakabili ikiwemo kuhakikisha wanalipwa madeni yao ya nyuma huku akiwataka kujenga umoja wao utakaowawezesha kuwasilisha changamoto zao wizarani kwa haraka.

Katika hatua nyingine, Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga kuhakikisha anawalipa wachimbaji wote wa visima na watafiti ambao wanaidai Serikali.

Miaka 8 bila Ngwea
CCM yalaani Catherine kuvamia msiba