WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa, amewapongeza wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Madagascar, jana Jumanne (Septemba 07) Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na dar24 Media baada ya mchezo huo, Waziri Bashungwa alisema amefarijika sana kwa ushindi huo wa Taifa Stars, kutokana na umuhimu wa mchezo huo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2022.

Alisema kwa matafanikio ya kupata alama tatu muhimu za mchezo huo dhidi ya Madagascar, , amewaandalia wachezaji wa Taifa Stars zawadi ya fedha taslimu (Shilingi milioni 10) kama ahsante ya kuwafurahishwa watanzania.

Alisema kwa namna alivyoiona Taifa Stars katika mchezo wa jana, ametambua timu hiyo inaendelea kuimarika na hana shaka kuelekea katika michezo ujayo ya kimataifa.

”Matarajio yangu ni kwamba wahakikishe wanapokuwa kambini wanafanya mazoezi vizuri na ningependa kutoa wito kwa Benchi la Ufundu  waendelee na moyo huo huo na vijana wetu waendelee kujituma.”

”Na mimi kwa furaha niliyonayo, kwa niaba ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mchezo mzuri walioweza kuuonesha tumewaandalia Shilingi milioni kumi kwa timu yote, ili kuwapongeza na mchezo waliocheza vizuri,” alisema Bashungwa.

Ushindi wa mabao 3-2 unaiwezesha Taifa Stars kuongoza msimamo wa kundi J, lenye timu za Benin, DR Congo na Madagascar.

Taifa Stars imefikisha alama 4 sawa na Benin baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya DR Congo uliomalizika kwa sare ya 1-1 na Madagascar uliomalizika kwa ushindi wa mabao 3-2.  

Manara: Fiston, Aucho na Djuma hawatacheza
Rais Samia apewa jina jipya na Machifu