Waziri wa Madini, Doto Biteko, amepiga marufuku shughuli za Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu unaofanywa na wachimbaji wadogo katika eneo la mgogoro la mlima Kaputa wilayani Chunya baada ya kubaini wananchi wa kata ya Chalangwa walitoa tarifa za uongo zilizosababisha Serikali kumzuia mwekezaji kuendeleza shughuli za uchimbaji katika mlima huo.

Uamuzi wa Waziri Biteko umetokana na kubainika kuwa wananchi wa kata hiyo walikuwa na chuki binafsi na mwekezaji aitwaye Joseph Mwazyele na wakatoa tarifa zisizo sahihi kwa Hayati Rais John Magufuli kuwa muwekezaji huyo anachimba madini ya dhahabu eneo lenye mradi wa matenki ya maji na makaburi.

Katazo hilo limetolewa jana Jumapili Juni 25, 2021 na waziri Biteko alipokuwa katika ziara eneo hilo iliyolenga kujiridhisha na uhalisia wa mgogoro baina ya mwekezaji na wananchi ambapo alibaini mgogoro huo ulipelekea mwekezaji huyo kusimamisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu tangu mwezi Mei 2019.

“Kwanza mmechuma dhambi, mlimdanganya Hayati Rais Magufuli kuwa mwekezaji huyo anachimba madini kwenye maeneo ya miradi ya matenki na makaburi, leo nimefika kuangalia uhalisia katika mlima huo na kubaini kuna udanganyifu kwani matanki ya maji yako mbali na eneo la muwekezaji na badala yake eneo lenye makaburi ambalo liko nje ya eneo la leseni ya mwekezaji pia limevamiwa na wachimbaji wadogo,” amesema Biteko.

Biteko amesimamisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo mpaka Serikali itakapoweka utaratibu mpya kuhusu eneo hilo.

Aidha, Biteko alitumia fursa hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka kwa kuwasilisha hoja za kuhitaji msaada wa Serikali kupitia Wizara ya Madini kuhusu mgogoro huo hivyo kuongeza msukumo kwa wizara kushughulikia suala hilo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon amepongeza maamuzi ya Waziri Biteko kufika kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa eneo hilo.

Amesema kuwa, mgogoro huo umesababisha shughuli nyingi za uchimbaji wa dhahabu katika eneo hilo la mlima kuwa na malalamiko mengi katika ofisi yake kama msimamizi.

“Sasa waziri kaagiza eneo hilo lisihusishwe tena na uchimbaji wa madini nitaweka ulinzi wa kutosha na vijana watakaothubutu kuingia na kuchimba wakibainika watawajibishwa, nasi tumejipanga kwani wananchi wa kata hii mnasifika kwa ukorofi,” amesisitiza Simon.

Simon amesema kuwa mgogoro huo kama Serikali waliufuatilia na kubaini mwekezaji huyo alikuwa anamiliki eneo hilo kihalali na si kweli kwamba mwekezaji alikuwa akichimba kwenye miradi ya maji na makaburi.

Kwa upandw wake Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kusubiri maamuzi ya Wizara ya Madini na kuwataka kukubaliana na maelekezo yaliyotolewa na waziri Biteko ili kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu na kukwamisha maendeleo ya Kijiji lakini pia umepelekea Serikali kukosa kodi.

Kasaka ameongeza kuwa, ujio wa waziri Biteko ili kujirishisha na kufanya maamuzi kwa kipindi hiki utaleta tija na kuchochea shughuli za maendeleo katika kata ya Chalangwa kupitia shughuli za uchimbaji madini zitakavyoendelea.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko alitembelea maeneo mbalimbali na kujionea namna shughuli za uchimbaji wa madini zinavyoendelea, kujionea teknolojia mpya na ya kisasa ya uchenjuaji wa dhahabu, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji katika eneo la Itumbi na Mgodi wa Apex resources Limited.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na mkuu wa wilaya ya Chunya, Mayeka Simon, Mbunge wa jimbo la Lupa Masache Kasaka, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chunya Sophia Kumbuli, Viongozi wa Chama na Serikali ya Vijiji.

Mbunge wa Nyamagana apongeza wananchi wa Nyamkanga
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 26, 2021