Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameziagiza hospitali zote nchini kuwa na mifumo rafiki ya kiutendaji katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa utaosaidia kupunguza muda wa kuwahudumia wananchi pindi wanapofika kupata huduma.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2021 wakati akifungua awamu ya kwanza ya mafunzo ya huduma bora kwa wateja iliyofanyika Mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali na watumishi kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali.

“Hospitali zote nchini kuwa na mifumo rafiki (systems and processes) ya kiutendaji katika kuwahudumia wananchi ili kupunguza muda wa huduma na hatimaye kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wananchi wanaopokea huduma hizo.”Amesema Dkt. Gwajima.

Ameendelea kwa kuagiza Hospitali zote nchini kuwa na mikataba iliyo wazi ya huduma bora kwa wateja iliyo hai inayotekelezwa na kufanyiwa tathimini, na kuweka wazi kuwa, msingi wa huduma bora kwa wateja unaanzia kwenye uwepo wa mkataba wa huduma kwa wateja.

Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kujifunza kwa makini na kupata ujuzi utakaosaidia kwenda kuboresha namna ya kutoa huduma katika maeneo ya kazi, na kuwataka waende kuwa Mabalozi wazuri kwa kuwaeleza watumishi wengine  kuhusiana na umuhimu wa huduma bora kwa mteja.

“Ninawasihi washiriki kujifunza na kupata ujuzi utakaosaidia kwenda kuboresha namna mnavyotoa huduma maeneo yenu ya kazi mlikotoka. Ninyi mkawe chachu ya kuwaleleza wenzenu waliobaki kuhusiana na suala hili.” Amesema Dkt. Gwajima.

Hata hivyo, ametoa wito kwa Hospitali zote nchini kuacha tabia ya kudhani wananchi wanaokuja kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma hawatambuhi haki zao na huduma bora ni zipi.

Mbali na hayo, ameziagiza hospitali zote nchini kuimarisha ushirikiano wa ndani ya taasisi/hospitali baina ya Watumishi kupitia idara na vitengo vilivyopo katika kuwahudumia wananchi.

“Tujifunze na tubadilike kuhusu kauli zetu na matendo yasiyofaa tunayowatendea  wananchi wanaokuja kupata huduma, huku tukiendelea kufuata kanuni, sheria, miongozo. Amesema Waziri Gwajima.

Tanzania yaikingia kifua Zimbabwe
Waziri Mkuu Majaliwa atoa agizo kwa jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi