Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanapata taarifa sahihi za ugonjwa wa uviko 19 kwa kusikiliza Serikali na Wataalamu wa afya ili kujiepusha na habari zisizo rasmi.

Waziri Gwajima ameyasema hayo wakati akipokea jumla ya chanjo Dozi 1,065,600 aina ya Sinopharm kutoka mpango wa COVAX Facility kwa ajili ya kuendelea kuwapatia wananchi chanjo dhidi ya UVIKO-19.

Akiongea wakati wa mapokezi ya chanjo hizo, Waziri Gwajima amesema chanjo hizo zimekuja na hivyo kuwapatia wananchi fursa ya kuchagua chanjo anayotaka kwani chanjo zote hizo ni salama ,zina ufanisi na ubora uliokubalika kisayansi na zimeonesha mafanikio makubwa katika kupunguza makali ya ugonjwa na kuepusha kifo.

“Ni dhahiri kuwa Serikali ya Tanzania imeonesha nia njema ya kuendelea kuwajali wananchi wake kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote kwenye sekta mbalimbali ikiwemo eneo la afya”.

Kwa upande wa Takwimu mpaka kufikia Oktoba 7, wananchi waliochanjwa wamefikia 760,962 sawa na asilimia 74.4 kwa Tanzania Bara na 10,800 Zanzibar na kuongeza kuwa mwitikio ni mkubwa na chanjo za awamu ya kwanza zinatarajia kumalizika mwisho wa wiki ijayo.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema Serikali inategemea kupokea chanjo za aina zingine katika wiki zijazo na itaendelea kutoa taarifa na utaratibu wa kila inapopokea ili wananchi wafahamu.

Vilevile Dkt. Gwajima amewasisitiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuelimishwa na kuhimizwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya ili wakapate elimu kuhusu umuhimu wa chanjo.

Mfahamu Abdulrazak Gurnah: Mwanafasihi aliebeba kidedea Tanzania Ulimwenguni
Fally Ipupa awapa shavu Wasanii wa Tanzania