Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo, amemuagiza Mhandisi Mkazi John Mageni na wakandarasi mradi wa Kimkakati wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji, kuhakikisha vyuma chakavu na taka za kielektroniki  zinazozalishwa kufuata utaratibu wa kimazingira, kuuzwa kwa wafashabiashara wenye vibali vya Serikali vya mazingira ikiwa ni pamoja na kibali cha ukusanyaji.

Ameyasema hayo mara baada kufanya ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa masharti yaliyowekwa katika cheti cha Tathmini ya Athari kwa mazingira kinachotolewa na Ofisi yake.

Aidha Waziri Jafo ameridhishwa na uzingatiaji wa Sheria ya mazingira katika kutekeleza mradi huo na maelezo yaliyotolewa na Mhandisi Mageni kuhusu hatma ya mashimo yanayochimbwa kwa ajili ya upatikanaji wa madini ujenzi ikiwemo mawe, kokoto na mchanga.

“Nimeridhika na maelezo ya wataalamu wetu kuwa mashimo haya yatatumika kama chanzo cha mazalia ya viumbe hai wa majini baada ya mradi kukamilika, nimefarijika sana,” Amesema Waziri Jafo.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka kusimamia kwa ukaribu na kufuatilia ajenda ya mazingira, uhifadhi na usimamaizi wa Mazingira katika ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.

 Akikagua mfumo wa Maji taka katika eneo la ujenzi, Waziri Jafo ameagiza Afisa Mazingira wa Mradi huo kuhakikisha anatunza takwimu za kiasi cha maji taka yanayozalishwa katika eneo hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo akikagua na kutoa maelezo kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya uzingatia wa Kanuni za Mazingira za Udhibiti wa Taka hatarishi na Taka za Kielekroniki za mwaka 2021. Waziri Jafo ameelekeza taka hizo ikiwa ni pamoja na chuma chakavu kuuzwa wa wafanyabiashara wenye vibali tu
Picha zikionyesha hatua mbalimbali za ujenzi wa Mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere. Ujenzi huo umefikia asilimia 54 ya utekelezaji kati ya asilimia 59 zilizokusudiwa na unaratajiwa kukamilika tarehe 14/06/2022.

Zuchu kufanya tamasha kubwa Zanzibar watakuwepo hawa
Mkakati wa 'KOPA MBUZI LIPA MBUZI' kuanza, chanjo za mifugo zatakiwa vijijini