Waziri wa Nishati, January Makamba, ameanza kazi rasmi katika wizara kwa kuwataka watendaji wa Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa.

Amesema hayo wakati akizungumza na uongozi wa Wizara pamoja Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kushika wadhifa huo na kuwasili katika ofisi za Wizara zilizopo katika Mji wa Magufuli Mtumba

Amewaeleza watumishi hao kuwa anahitaji kuona matokeo chanya katika utendaji kazi pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Aidha, amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kusukuma mbele Sekta ya Nishati kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa kwakuwa sekta hiyo ni mhimili muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini( REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( Ewura), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja( PBPA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Mafuta ( PURA), kuhakikisha zinafanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya nchi na watanzania kwa jumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ametoa pongezi kwa Waziri wa Nishati kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na kwamba watumishi wa Wizara wamempokea kwa moyo mkunjufu.

Vilevile amemuhakikishia Waziri Makamba, kuwa watumishi wa Wizara pamoja na Tasisi zilizo chini ya wizara hiyo zitatoa ushirikiano mkubwa wa kiutendaji katika kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele na kunufaisha Taifa na watanzania kwa jumla.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Viongozi Waandamizi wa wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 14, 2021
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) yapigwa msasa