Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amemkabidhi rasmi majukumu Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Ally Mayay, baada ya kumteua juzi Jumanne (Septemba 19).

Ally Mayay ambaye aliwahi kucheza soka katika klabu za CDA ya Dodoma na Young Africans ameteuliwa kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Yusuph Omary Singo aliyepangiwa majukumu mengine na uteuzi huo umeanza kazi rasmi leo Septemba 20, 2022.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Waziri Mchengerwa amemuagiza Ally Mayay kushirikiana na Shirikisho la Soka TFF ili kujenga misingi ya kuwa na timu bora za Taifa kwa kuibua vipaji vya vijana nchi nzima.

Waziri Mchengerwa amesema katika jukumu hilo la kwanza kwa Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Serikali itaunga mkono kwa asilimia 100, ili kufanikiwa mpango wa kuwa na timu za taifa Bora na Imara ambazo zitakuwa na uwezo wa kupambana na yoyote Afrika na Duniani kwa ujumla.

“Sisi kama Serikali tutamuunga mkono katika yote atakayoyafanya kwenye kuleta mapinduzi katika sekta ya michezo, kama utahitaji usaidizi wa kwenda popote pale ndani na nje ya nchi hii kwa ajili ya kuwafuatilia vijana wenye vipaji, tutakuwezesha,”

“Watanzanai wanataka kuwa na timu nzuri zitakazowapa furaha wakati wote, kwa hilo kila mmoja wetu anakubali kwa miaka kadhaa tumekua wasindikizaji katika Michuano mbalimbali inayozihusisha timu zetu za taifa, imefikia hatua kila mtanzania amekua akibashiri kufungwa kwa timu zetu zinapokua katika majukumu ya mapambano,”

“Sasa hili tunapaswa kulikataa kwa kuwa na timu zitakazopambana na kuleta ushindi, na njia sahihi ni kuwa na timu Bora ambazo zitaboreshwa kwa misingi ya kuwa na wachezaji vijana na wenye vipaji vitakavyofanikisha lengo la kuwafurahishwa watanzania wote.” amesema Waziri Mchengerwa

Kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Mendeleo ya Michezo, Ally Mayay aambaye ameitumikia Taifa Stars wakati wakicheza soka, alikuwa Afisa Mwandamizi katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, pia alikua akichambua michezo katika kituo cha Televisheni cha Azam TV.

Simba SC yahofia hujuma Angola
Twaha Kiduku aahidi makubwa Mtwara