Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amempa mwezi mmoja mkandarasi anayejenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilometa mbili inayounganisha daraja la Nyerere na barabara ya Kibada-Feri iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, kukamilisha kazi  hiyo hadi tarehe 31 Agosti, mwaka huu, ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wanaovuka  daraja hilo.

Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akikagua  ujenzi wa barabara hiyo na kujionea uendeshaji wa shughuli  katika daraja la Nyerere.

“Hii barabara ni ya msingi kwani kutokamilika kwake ndo maana hata magari madogo hayapendi kutumia hii njia, Mkandarasi huyu ameomba mara mbili kuongezewa muda kukamilisha kazi hii na sasa tunampa muda tena, nataka kazi hii ikamilike kwani baada ya  kukamilisha ujenzi wa daraja hili tulitegemea kuwa mapato tutakayo kusanya hapa yatatuwezesha kulipa gharama tulizotumia kuwekeza na kujenga daraja hili, lakini nimejaribu kuangalia makusanyo ya tangu mwaka 2016/2017 na mwaka 2017/2018 inakuwa kidogo sana ikilinganishwa na mapato ya mwaka 2016, hili lazima liangaliwe,   tunataka daraja hili liendelee kutoa huduma na liendelee kuleta faida kwenye mfuko na ukizingatia fedha  hizi ni za wanachama zilizotumika” Amesema Mhagama.

Mhagama amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha unawekwa mfumo bora wa utambuzi wa vyombo vya usafiri vinavyovuka darajani hapo ili kujua gharama halisi ya tozo kwa vyombo vya usafiri vinavyovuka darajani  hapo na kuepuka upotevu wa mapato kutokana na kutokuwa na mfumo wenye kutambua tozo halisi kwa vyombo hivyo.

Kwa upande wao Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Eriona na Mkandarasi wa barabara hiyo, Mhandisi Jamal Mruma wote kwa pamoja wamemuhakikishia Waziri kutekeleza maagizo hayo kwa wakati.

Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya China Railway Construction Agency Group, kwa gharama ya shilingi bilioni 21.1, ambapo tayari kampuni hiyo imeshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 10.5.

Kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza mapato yanayotokana na tozo za vyombo vya usafiri vinavyovuka Darajani hapo ambapo tangu Daraja hilo lianze kufanya kazi mwezi Mei, 2016 hadi Juni 2018,  takribani shilingi bilioni 17.1 zimekusanywa na  kwa wastani kila mwezi mapato ya shilingi milioni 600 hukusanywa.

 

 

Waziri Mkuu ateta haya na balozi wa Tanzania nchini China
Arsene Wenger kukabidhiwa kikosi cha Japan?