Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga awasilishe kwake taarifa za utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kata ya Rutamba.

Ametoa agizo hilo Agosti 23 wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye kijiji cha Rutamba akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma za jamii mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Lindi amesema kuwa mradi wa kata hiyo unakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu na ukarabati wake unahitaji bajeti ya  sh. milioni 75, ambazo wameziomba kutoka Wizara ya Maji.

”Miradi yote ambayo gharama zake ziko chini ya sh. milioni 100 inatakiwa itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika, miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa, mradi wa sh. milioni 75 unaomba fedha wizarani? huu ni uvivu,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema suala la huduma ya maji limewekewa msisitizo na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama karibu na makazi yao.

Video: Mawakili 15 wamwekea Tundu Lissu pingamizi | Uchaguzi Serikali za mitaa Novemba 24
Video: Kaka yake Lissu afunguka, 'Hii kesi sio ya hovyo'