Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameendeleza kasi ya serikali ya awamu ya tano iliyoanzishwa na rais John Magufuli ambapo amewabana watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kujieleza kwanini mradi wa mabasi ya mwendo kasi Dar es Salaam haujaanza kutekelezwa.

Waziri Mkuu alitoa tamko hilo jana alipofanya kikao maalum na watendaji wa ofisi hiyo ambapo alitoa hadi saa nne asubuhi ya leo apewe maelezo ya kutosha ya sababu za mradi wa mabasi ya mwendo kasi jijini humo kutoanza kutoa huduma kwa wananchi licha ya mabasi hayo 140 kuwasili nchini miezi miwili iliyopita.

“Natoa hadi saa nne asubuhi muwe mmeniletea details (maelezo) kwanini hadi sasa mabasi hayo hayafanyi kazi,” alisema Waziri Mkuu. “Nataka ushirikiano kwenu kwa sababu watanzania wanajua ni TAMISEMI, sasa hawajui huku ndani kama kuna vitengo vingine vinavyozuia vingine.”

Awali, serikali ilitangaza kuwa mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (DAT) ungeanza Oktoba 2 mwaka huu. Tayari hatua ya majaribio ilifanyika na kutangazwa kuanza kuwapa mafunzo madereva wa mabasi hayo ili kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.

Mabasi

Hata hivyo, ukimya ulitawala mradi huo ambao umewekwa kando bila maelezo huku wananchi wa jiji la Dar es salaam wakiona ndoto yao ya kupanda mabasi hayo mwaka huu ikififia bila kupewa maelezo ya kutosha.

 

Mahakama Yatupilia Mbali Pingamizi La Polisi Mwanza Kuhusu Kesi Ya Mawazo
Unaweza Kuigiza Kama Sokwe? Unatafutwa Kwa Filamu Hii Ya Kimataifa